OPERESHENI ANWANI ZA MAKAZI UMELETA MAFANIKIO MAKUBWA, ZAIDI YA ANWANI ZA MAKAZI MILIONI 12.3 ZILISAJILIWA NA TAARIFA ZAKE KUHIFADHIWA KWENYE MFUMO WA NaPA -KATIBU MKUU ABDULLA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Khamis Abdulla amesema Operesheni Anwani za Makazi ilikuwa na mafanikio makubwa ambapo zaidi ya Anwani za Makazi milioni 12.3 zilisajiliwa na taarifa zake kuhifadhiwa kwenye Mfumo wa Anwani za Makazi unaojulikana kwa jina la NaPA, na pia majengo yalibandikwa vibao vya namba za nyumba pamoja na nguzo za majina ya Barabara ziliwekwa kwenye mitaa yetu hapa nchini.
.
Abdulla ameyasema hayo leo April 16,2024 alipokuwa kwenye hafla ya kukabidhi vifaa na kuzindua Majaribio ya kutoa Huduma ya Barua ya utambulisho wa Mkazi kupitia Mfumo wa Kidijitali wa Anwani za Makazi tukio lililofanyika katika Ukumbi wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
.
Amesema kuanzisha mfumo wa Anwani za Makazi ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003; makubaliano ya Kikanda kupitia Umoja wa Posta Afrika yaani Pan Africa Postal Union -PAPU; makubaliano ya Kimataifa kupitia Umoja wa Posta Duniani yaani Universal Postal Union - UPU; na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya miaka mitano,2020–2025, na hata hivyo,mpango huo haukukamilika kwa wakati kutokana na kukosa jitihada za pamoja na ufinyu wa bajeti.
.
Katibu Mkuu Abdulla amesema ni dhamira ya Serikali ya kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo ili kuondoa usumbufu kwa wananchi wa kufuata barua kwenye ofisi za Serikali za Mitaa,Kuondoa mianya ya udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wananchi, kuondoa msongamano kwenye ofisi za watendaji na hivyo kuongeza ufanisi katika kutoa huduma.
.
"Kwa msingi huo mwananchi sasa atatumia simu ya mkononi kuomba barua hiyo bila kulazimika kufika kwenye ofisi ya mtendaji. Hivyo, nitumie fursa hii kuujulisha Umma kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha anafahamu Anwani yake ya Makazi na kwamba taarifa zake zimesajiliwa kwenye Mfumo wa NaPA ambalo ni daftari la kidijitali la ukazi kama nilivyoeleza hapo wali" alisema Abdulla.
.
Aidha,Abdulla amesema Mkakati wa Wizara ni kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na Anwani ya Makazi ambayo ataitumia katika kujitambulisha,ili kufikia dhamira hiyo wamejipanga kujenga uwezo kwa watendaji wa Kata, Mitaa, vijiji na shehia kote nchini.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

