KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA AFYA NA UKIMWI YATEMBELEA BMH, YAPONGEZA MAPINDUZI YA UWEKEZAJI SEKTA YA AFYA,YASISITIZA UMUHIMU WA BIMA YA AFYA KWA WOTE
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI leo imefanya ziara katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na kupongeza mapinduzi makubwa yaliyofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya Afya na hususani Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Dkt. Johannes Lukumay amesema kuwa Kamati imeridhishwa na hatua zilizofikiwa na BMH za kutoa huduma 20 za Ubingwa, 17 za Ubingwa bobezi zikiwemo upandikizaji Uloto kwa watoto wenye Sikoseli na Upandikizaji Figo, huduma ambazo hapo awali Watanzania walilazimika kwenda kuzifuata nje ya nchi kwa gharama kubwa.
Aidha, alisisitiza Serikali kuendeleza mkazo wa suala la Bima ya Afya kwa wote na Viwanda vya kuzalisha dawa na Vifaa tiba.
"Tunaipongeza Serikali, uelekeo katika Sekta ya Afya sasa ni kuanzisha viwanda vyetu vya kutengeneza dawa na vifaa tiba ili kupunguza utegemezi kutoka nchi za nje, viwanda vya madawa na vifaa tiba vitasaidia pia kuzalisha ajira kwa vijana na kuchangia uchumi" alisisitiza Dkt. Lukumay
Aliongeza kuwa Serikali iendelee kuweka mkazo wa Bima ya Afya kwa wote, itasaidia makundi yote katika jamii kuwa na uhakika wa kupata huduma za Afya hususani matibabu ya magonjwa yanayosumbua na yenye gharama kubwa za matibabu kama ya Sikoseli, Figo, Moyo, Kisukari na Mifupa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi amesisitiza kuwa Wizara itahakikisha ujenzi wa mradi wa kituo cha Umahiri cha Mafunzo na Matibabu ya Saratani unaojengwa BMH kwa thamani ya shilingi Bil. 32 unakamilika kwa wakati na vifaa vya kutolea huduma vinawekwa baada tu ya ujenzi kukamilika, lengo la Serikali likiwa kuhakikisha huduma za Kibingwa Bobezi za Saratani zinapatikana kwenye kanda zote nchini.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi amesema kuwa asilimia 60 ya huduma 20 za Ubingwa na 17 za Ubingwa Bobezi zimeanzishwa wakati wa utawala wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwa sasa BMH imewekeza kwa kiasi kikubwa katika suala zima la huduma bora kwa mteja.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

