logo

MASHINDANO YA UJUZI ‎KITAIFA 2026 YAANZA RASMI

Mashindano ya Ujuzi kitaifa 2026 , ngazi ya Kanda, yameanza rasmi yakiwakutanisha wanafunzi wa vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi wakichuana katika fani mbalimbali.

‎Mnamo tarehe 8 Juni, 2026, wanafunzi wa fani ya Upishi walishiriki mchujo wa ngazi ya kanda uliofanyika katika chuo cha VETA cha Hoteli na Utalii, Njiro- mkoani Arusha.

‎Mashindano haya yanaratibiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

‎Haya ni mashindano ya kwanza kufanyika tangu Tanzania ipate uanachama wa Worldskills Africa.

‎Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora NACTVET, Dkt. Jofrey Oleke, alisema kuwa mashindano hayo, yanalenga kuhamasisha maendeleo ya ujuzi miongoni mwa vijana kupitia elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, ili kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Dkt. Oleke aliongeza kuwa, washindi ngazi ya kanda watashiriki mashindano hayo ngazi ya Kitaifa mwezi Agosti, 2026, ambapo washindi wa kitaifa watapata fursa ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Kimataifa ngazi ya Afrika.

‎Maeneo ya ujuzi yanayoshindaniwa ni pamoja na Upishi, Uhandisi wa Mitambo, Uwekaji wa Vigae Sakafuni, Uchomeleaji na Uungaji Vyuma, Ushonaji na Ubunifu wa Nguo, Mtandao wa Vitu (IoT), Mekatroniki, Urembo Tiba na Ufundi Umeme.

‎Kwa upande wake, mmoja wa washiriki wa mashindano hayo, Prudence Musoni alisema kuwa ushiriki wake umemwezesha kujifunza mbinu mpya za upishi na kuongeza uzoefu wa vitendo na kuimarisha uwezo wake kitaaluma.

‎Mashindano ya Ujuzi Kitaifa yanatarajiwa kuwa chachu ya kuibua vipaji, kuhamasisha ubunifu na kuimarisha ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn