SERIKALI KUZIBA NA MIKAKATI YA KUPAMBANA NA UTAKATISHAJI FEDHA
Ili kupunguza matumizi ya fedha taslimu na kuziba mianya ya utakatishaji wa fedha haramu, Serikali imeweka utaratibu wa malipo kwa njia za kidijitali katika miamala mbalimbali nchini.
Utaratibu huo umewekwa kupitia marekebisho ya Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, Sura ya 442 na kutungwa kwa Amri ambayo inabainisha miamala inayopaswa kufanyika kwa njia ya kidijitali, kwa mujibu wa Amri hiyo, mtu yeyote anayefanya au kupokea malipo katika miamala iliyobainishwa anapaswa kutumia njia ya kielektroniki.
Akizungumza wakati wa mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kuhusu mabadiliko yaliyotokana na Sheria ya Fedha ya mwaka 2026, Mkurugenzi Msaidizi wa Divisheni ya Uandishi wa Sheria kutoa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD), Bi. Chresencia Mathayo alisema hatua hiyo inalenga kujenga mfumo wa malipo ulio salama na unaoweza kufuatiliwa kwa urahisi hivyo kusaidia kuziba mianya ya utakatishaji wa fedha haramu nchini.
“Matumizi ya njia za kidijitali katika miamala yanarahisisha ufuatiliaji wa malipo, yanaongeza usalama wa fedha na yatasaidia kuziba mianya inayoweza kutumika katika utakatishaji wa fedha haramu, ukwepaji wa kodi na vitendo vingine vya uhalifu wa kifedha,” alisema Bi. Chresencia.
Kwa mujibu wa Amri hiyo, njia zinazotambuliwa kuwa za kidijitali zinajumuisha fedha kwa simu, uhamisho wa fedha kupitia benki, kadi za malipo, mashine za malipo (POS), huduma za benki kwa njia ya mtandao au simu pamoja na mifumo ya malipo ya Serikali.
Bi. Chresencia alieleza kuwa Amri hiyo imebainisha miamala yote ambayo inapaswa kufanyika kidijitali.
“Miongoni mwa miamala ambayo ni lazima kufanyika kwa njia ya kidijitali ni pamoja na malipo ya ada za shule, malipo ya nauli kwenye vyombo vya usafiri (mabasi ya mwendokasi, madaraja, vivuko, teksi mtandao, mabasi ya masafa marefu, usafiri wa anga na reli), huduma kwenye maduka makubwa (supermarket), huduma za malazi na chakula kwenye mahoteli na migahawa, huduma za kitalii, malipo ya kupangisha au kuuza jengo, shamba au kiwanja, malipo ya uuzaji na ununuzi wa magari na malipo yanayofanyika kupitia vyama vikuu vya ushirika na Vyama vya Ushirika vya Mazao na Masoko (AMCOS) katika mazao ya kimkakati,” amesema Bi. Chresencia.
Mkurugenzi Msaidizi wa Divisheni ya Uandishi wa Sheria OCPD, aliendelea kwa kusema kuwa sambamba na hatua hiyo, Kanuni za Utoaji wa Leseni za Biashara zimerekebishwa pia ili maombi ya leseni mpya na maombi ya kuhuisha leseni kwa wafanyabiashara wote yaambatishwe na uthibitisho wa matumizi ya mfumo au kifaa cha kupokea malipo kwa njia ya kidijitali, ikijumuisha Lipa Namba au TANQR.
“Kwa wafanyabiashara wote ambao bado hawana njia za malipo ya kidijitali watashindwa kuhuisha leseni zao za biashara pindi muda wake unapoisha mpaka pale watakapokuwa na njia za malipo ya kidijitali, hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa miamala katika biashara hizo inapitia katika mifumo rasmi ya kifedha,” ameendelea Bi. Chresencia.
Bi. Chresencia alisema maboresho hayo hayalengi tu ukusanyaji wa mapato, bali pia kupunguza gharama na hatari zinazotokana na matumizi ya fedha taslimu, ikiwemo gharama za kutunza na kusafirisha fedha pamoja na hatari ya wizi na upotevu wa fedha.
Mabadiliko hayo yameanza kutumika rasmi Julai 1, 2026, hivyo wananchi, wafanyabiashara na watoa huduma wanahimizwa kujiandaa na kutumia njia rasmi za malipo ya kidijitali katika miamala iliyobainishwa.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

