DKT.MSONDE: MFUKO WA BARABARA NI NGUZO YA MATENGENEZO YA BARABARA NCHINI
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, amesema Mfuko wa Barabara una mchango mkubwa katika kuhakikisha barabara nchini zinaendelea kuwa salama, zenye ubora na zinazopitika wakati wote kupitia ufadhili wa shughuli za matengenezo.
Dkt. Msonde ameyasema hayo alipotembelea banda la Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela, jijini Dodoma, ambapo alipata elimu kuhusu majukumu ya Mfuko wa Barabara na namna unavyowezesha utekelezaji wa matengenezo ya barabara nchini.
Ameeleza kuwa barabara, kama ilivyo miundombinu mingine, hupungua ubora kadri zinavyoendelea kutumika, hivyo zinahitaji matengenezo ya mara kwa mara ili zisiharibike zaidi. Alisisitiza kuwa kufanya matengenezo kwa wakati huongeza maisha ya barabara, hupunguza gharama za ukarabati mkubwa na kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma za usafiri na usafirishaji kwa ufanisi.
Aidha, amesema fedha za Mfuko wa Barabara zinatokana na mchango wa wananchi, hivyo ni muhimu kila Mtanzania kushiriki katika kuzitunza na kuzilinda barabara ili thamani ya fedha zinazowekezwa iendelee kuonekana kupitia miundombinu bora na ya kudumu.
Dkt. Msonde pia amebainisha kuwa katika mwaka huu wa fedha Serikali imeelekeza fedha zinazohusu matengenezo ya barabara kupelekwa moja kwa moja kwenye Mfuko wa Barabara, hatua itakayorahisisha uratibu wa shughuli za matengenezo na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali hizo kwa manufaa ya wananchi.
Maonesho ya Nanenane mwaka 2026 yanaendelea chini ya kaulimbiu isemayo, “Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa 2050.”
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

