BALOZI BYAKANWA ATEMBELEA BENJAMIN MKAPA HOSPITAL JIJINI DODOMA
Balozi wa Tanzania nchini Burundi Mhe. Gelasius Byakanwa ametembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na kuwaona watoto kutoka nchini Burundi waliofanyiwa upasuaji wa moyo hospitalini hapo.
Balozi Byakanwa ameelezea kuridhishwa na kuimarika kwa Afya za watoto hao waliofanyiwa upasuaji wa moyo.
"Nimewatembelea wodini watoto wale waliofanyiwa upasuaji, hali zao zinaendelea vizuri sana, kwa mtu wa kawaida ukiwaona kwa sasa unaweza usiamini kama walikuwa wanaumwa na changamoto za moyo hivyo niwapongeze timu za Madaktari na Wauguzi wa BMH na JKCI kwa kazi mliyoifanya ya kitaalamu kuwatibu watoto hao" alisisitiza Mhe. Byakanwa.
Aliongeza kuwa, Serikali imefanya kazi kubwa ya kuwekeza kwenye miundombinu, vifaa tiba na kusomesha rasilimali watu kuzalisha mabingwa bobezi ambao leo wanaiheshimisha nchi yetu kwa kutoa huduma za kibobezi hata kwa nchi zinazotuzunguka.
Aidha, aliipongeza BMH kwa kudhihirisha huduma bora zenye hadhi ya kimataifa na kubainisha kuwa huo ni mwanzo wa kufungua milango kwa watu wa kimataifa na wageni mbalimbali kuja nchini kupata huduma za matibabu ya kibobezi.
"Jambo la kufurqhisha ni kwamba BMH mmeshaandaa eneo maalumu la kuwapokea wageni wa kimataifa na kuwapatia huduma za Afya, nitoe wito kwa Menejimenti na Watumishi wote wa BMH kulinda sifa nzuri ya BMH kwa kuendelea kutoa huduma bora na ukarimu kwa wagonjwa" alisisitiza Mhe. Byakanwa.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi ameshukuru ushirikiano baina ya Tanzania na Burundi na kuahidi BMH iko tayari kuendelea kutoa huduma za tiba utalii kwa wageni kutoka nchini Burundi kwenye matibabu ya ubobezi ya moyo, saratani, upandikizaji figo, upandikizaji uloto na viungo vingine sambamba na matatizo ya mfumo wa mkojo.
Prof. Makubi amemshukuru Balozi Byakanwa na wadau wengine waliofadhili kambi ya matibabu ya BMH iliyofanyika Burundi mwaka jana na hivi sasa kuwezesha watoto kutoka Burundi kuja BMH kuendelea na matibabu ya upasuaji.
.
Nae Bw. Shedrack Nzigiyimana akiwakilisha Wazazi ambao watoto wao tayari wamefanyiwa upasuaji wa moyo, amemjulisha Mhe.Balozi kuwa, tangu wamewasili BMH wamepokelewa kwa ukarimu, wamepewa huduma za kiwango cha juu ambazo zimesaidia watoto wao kurejea kwenye Afya njema baada ya kukamilisha upasuaji.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

