TANROADS YATAKIWA KUSHIRIKIANA NA WADAU KUTUMIA HUDUMA ZA MAABARA ZAKE ZA KISASA
NAIBU Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya, amezungumzia umuhimu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kushirikiana na sekta binafsi na taasisi za elimu ya uhandisi katika kuendesha maabara zake za kisasa.
Hatua hiyo itaiwezesha TANROADS kuongeza mapato, kuimarisha huduma za kitaalamu na kuifanya Taasisi hiyo kuwa kitovu cha umahiri katika upimaji wa vifaa vya ujenzi wa barabara nchini na ukanda wa Afrika Mashariki.
Eng. Kasekenya amesema hayo leo wakati wa ziara yake kukagua maendeleo ya ujenzi wa Makao Makuu ya TANROADS jijini Dodoma.
Ameitaka TANROADS kuhakikisha viongozi wake wakuu na watumishi wanaopaswa kuhamia Makao Makuu ya nchi wanakamilisha uhamisho wao ifikapo mwisho wa Agosti mwaka huu.
Amemtaka Mkandarasi CRJE East Africa Ltd. anayejenga jengo hilo ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 85 kuongeza kasi ili likamilike kwa wakati.
"Tunapoelekea katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ni muhimu Taasisi za umma kuangalia namna ya kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza tija kwa umma hivyo TANROADS ina maabara za kisasa ambazo zinaweza kutumika kutoa huduma za kibiashara na kitaalamu kwa taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi," amesisitiza Naibu Waziri Kasekenya.
Aliongeza kuwa ushirikiano, ubunifu, uadilifu na moyo wa kujituma kutaifanya TANROADS kuwa kituo cha umahiri katika upimaji wa vifaa vya ujenzi wa barabara na kuongeza uwezo wa wataalamu wa ndani kupitia ubadilishanaji wa uzoefu na teknolojia.
Eng. Kasekenya amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejidhatiti kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa ili kuimarisha uwezo wa Taasisi za Serikali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
"Serikali imehakikisha TANROADS inapata eneo kubwa pamoja na majengo na maabara za kisasa zinazokwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia duniani," amesema Eng. Kasekenya.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Eng. Zuhura Amani, amesema mradi huo wenye thamani ya Shilingi bilioni 49.72 unatekelezwa na kampuni ya CRJE East Africa Limited chini ya usimamizi wa Tanzania Building Agency (TBA) katika eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 78,474.
Eng. Zuhura amesema tayari takribani watumishi 220 wa TANROADS wamehamia Dodoma kufuatia utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuhamishia Taasisi zake Makao Makuu ya nchi.
Aliongeza kuwa mradi huo umechangia matumizi ya malighafi zinazozalishwa nchini, hatua iliyonufaisha viwanda vya ndani, huku ukitoa ajira 211 kwa Watanzania na ajira kwa wataalamu wanane kutoka nje ya nchi.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

