logo

ULEGA AAGIZA TANROADS KUHARAKISHA MATENGENEZO YA BARABARA MANYARA

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametoa maelekezo kwa mameneja wa TANROADS kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara zinatumika kwa kazi hiyo pekee na si vinginevyo.

‎Pia waziri huyo ametaka kusiwe na ucheleweshaji wa utekelezaji wa kazi hizo kwa kisingizio cha taratibu za kiutendaji, ili wananchi waendelee kupata huduma bora za miundombinu kwa wakati.

‎Ulega ametoa maelekezo hayo wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Manyara, ambapo amekagua ujenzi wa barabara ya Karatu- Mbulu - Hydom - Sibiti - Meatu - Lalago - Maswa (km 389) sehemu ya Mbulu - Garbabi na Labay - Hydom kwa kiwango cha lami pamoja na barabara ya zege ya Mbuyu wa Mjerumani - Mlima Magara hadi Mbulu.

‎“Fedha zinakuja kwa ajili ya barabara za wananchi. Sitaki kusikia fedha zimefika mkoani halafu naambiwa mchakato unaanza au unaendelea wakati barabara ziko katika hali mbaya. Sitavumilia hali hiyo," amesema Ulega.

‎Ulega ameeleza kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa ubora na kwa wakati pamoja na kusimika taa za barabarani katika barabara za Mbulu ili kuchochea maendeleo ya wananchi.

‎Aidha, Waziri Ulega amesema kuwa viongozi na watendaji watakaoshindwa kusimamia matumizi ya fedha za barabara kwa wakati na kwa ufanisi wataondolewa katika nafasi zao.

‎Ulega amesema barabara hiyo ni muhimu na ni ya kimkakati kwani sehemu ya mtandao muhimu wa usafiri unaounganisha mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Shinyanga na Simiyu, hivyo inapaswa kukamilishwa kwa wakati.

‎"Nimekagua mradi kutoka Mbulu kuelekea Garbabi kupitia Tlawi na kujionea maendeleo yake. Niwahakikishie Serikali itaendelea kuujazia fedha mradi huu ili mkandarasi akamilishe kazi kwa viwango vinavyotakiwa," amesema Ulega.

‎Katika hatua nyingine, Ulega ameiagiza TANROADS, wasimamizi wa miradi na wakandarasi wote nchini kuhakikisha ujenzi wa barabara unazingatia viwango vya ubora ili fedha za umma zitoe thamani inayostahili na miundombinu idumu kwa muda mrefu.

‎"Hatutakuwa tayari kuona barabara mpya imejengwa mwaka huu, halafu baada ya mwaka mmoja inaanza kuwa na mashimo. Watanzania hawafurahii jambo la namna hiyo," amesema.

‎Kadhalika, amewataka wasimamizi wa miradi kuepuka kuwa na ukaribu unaoweza kuathiri uwajibikaji wao kwa wakandarasi, akisisitiza kuwa wanapaswa kusimamia miradi kwa haki, weledi na uaminifu.

‎Aidha, amesema kuanzia mwaka wa fedha 2026/27 atapima utendaji wa Mameneja wa TANROADS wa mikoa yote kwa kuzingatia ubora wa ujenzi wa barabara na ufanisi wa matengenezo katika maeneo yao.

‎Vilevile, ameelekeza mkandarasi aliyekuwa akijenga sehemu ya barabara ya zege katika eneo la Mlima Magara kurejeshwa ili akamilishe kazi kwa viwango vinavyotakiwa.

‎Pia, ameagiza mkandarasi anayesimamia barabara ya Garbabi–Labay kufanya matengenezo ya mara kwa mara ili barabara hiyo iendelee kupitika na kuondoa usumbufu kwa wananchi, ikiwemo kuepusha kupanda kwa nauli.

‎Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Manyara Mhandisi Dutu Masele ameeleza kuwa ujenzi wa barabara sehemu ya kwanza inayoanzia Mbulu - Garbabi (km 25) umefikia asilimia 45 na sehemu ya pili ya barabara hiyo inayoanzia Labay - Hydom (km 25) ambapo hadi sasa utelelezaji wamradi umefikia 17 na sehemu zote hizo zinatekelezwa na Mkandarasi Jiangxi Geo - Engineering Group Corporation kwa utaratibu wa Sanifu Jenga.

‎Kwa upande wao, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Dkt. Emmanuel Nuwas, na Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini, Issaay Zacharia Paulo, walisema wananchi wao wamekuwa wakihitaji kwa muda mrefu barabara ya lami kutokana na umuhimu wake kwa shughuli za kilimo, ufugaji na biashara, pamoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya na elimu.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn