logo

AFYACHECK YAWAJENGEA UWEZO WAZAZI WA WATOTO WENYE ULEMAVU USIOONEKANA DODOMA

Mkurugenzi wa Taasisi ya AfyaCheck, Dkt. Isaac Maro, amefungua rasmi mafunzo maalum ya siku tatu kwa wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu usioonekana (Neurodevelopmental Disorders), yanayofanyika katika Hoteli ya Zabibu jijini Dodoma.

‎.

‎Akizungumza baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo, Dkt. Maro amewahimiza wazazi na walezi wenye watoto wanaokabiliwa na changamoto za maendeleo ya ubongo na mfumo wa fahamu kujitokeza kwa wingi ili kupata elimu itakayowasaidia kuwalea watoto hao kwa ufanisi zaidi.

‎.

‎Ametaja baadhi ya changamoto zinazojumuishwa katika kundi hilo kuwa ni Usonji (Autism), Down Syndrome, ADHD, ADD, Utindio wa Ubongo (Cerebral Palsy) pamoja na hali nyingine zinazohusiana na maendeleo ya mtoto.

‎.

Dkt. Maro amesema mafunzo hayo, yanayoendelea kuanzia Juni 25 hadi 27, 2026, yamepata mwitikio mzuri kutoka kwa wazazi na walezi, ambao wamepata fursa ya kujifunza kuhusu namna ya kutambua mahitaji ya watoto wao na mbinu bora za kuwalea ili waweze kujitegemea wanapokuwa watu wazima.

‎.

‎Ameeleza kuwa siku ya pili ya mafunzo itajikita katika masuala ya lishe na maeneo mengine muhimu yanayohusu ustawi wa watoto hao, huku wataalamu wakitoa elimu inayomwangalia mtoto kwa mtazamo mpana ili kusaidia maendeleo yake kwa ujumla.

‎.

‎“Tunaamini mzazi anapopata uelewa sahihi wa mahitaji ya mtoto wake, inakuwa rahisi zaidi kumpatia msaada unaohitajika na kumwezesha kukua vizuri na kujitegemea,” alisema Dkt. Maro.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn