logo

TEMESA YAJIVUNIA MAFANIKIO MAKUBWA NDANI YA MIAKA 20 ‎

WAKALA wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) umeadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake kwa kujivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utoaji wa huduma za ufundi, usimamizi wa mitambo na maboresho ya miundombinu ya umeme nchini.

‎Akizungumza katika hafla fupi ya maadhimisho hayo iliyofanyika Juni 23,2026 katika ofisi za TEMESA jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala huo Kheri Mahimbali, amesema taasisi hiyo imeendelea kupanua wigo wa huduma zake kwa kushirikiana na sekta binafsi katika maeneo ya matengenezo ya magari, mitambo pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiufundi.

‎Mahimbali amesema mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka 20 yamechangiwa na juhudi za wafanyakazi wa TEMESA pamoja na ushirikiano mzuri kati ya taasisi hiyo, Serikali na sekta binafsi.

‎Ameeleza kuwa TEMESA imeendelea kuboresha miundombinu ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo uwekaji na matengenezo ya taa za barabarani, hatua ambayo imeimarisha huduma kwa wananchi na kuongeza usalama katika maeneo ya mijini na vijijini.

‎“Katika kipindi hiki cha miaka 20, tumeshuhudia ukuaji mkubwa wa taasisi yetu kupitia utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya kiufundi na upanuzi wa huduma zinazolenga kukidhi mahitaji ya wananchi na taasisi za umma,” amesema Mahimbali.

‎Aidha, amesema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuelekeza taasisi za umma kujiendesha kwa ufanisi, kuongeza tija na kuchangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya uchumi wa Taifa.

‎Kwa mujibu wa Mahimbali, TEMESA itaendelea kuimarisha shughuli zake za kibiashara kwa lengo la kuongeza mapato yatakayosaidia kuboresha mazingira ya kazi pamoja na maslahi ya watumishi wake.

‎Ametumia nafasi hiyo kuwapongeza wafanyakazi wa TEMESA kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha majukumu ya taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka 20, huku akiahidi kuendelea kushughulikia maslahi yao ili kuongeza ari ya kazi na ufanisi katika utoaji wa huduma.

‎Maadhimisho hayo yamekuwa fursa ya kutathmini mafanikio, changamoto na mwelekeo wa TEMESA katika kuendelea kutoa huduma bora za ufundi na umeme kwa maendeleo ya Taifa.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn