MABORESHO YA KIWANJA CHA NDEGE KIGOMA YAFIKIA ASILIMIA 60
Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imesema kuwa mradi wa ukarabati na uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege Kigoma umefikia asilimia 60 ya utekelezaji.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Elisony Mweladzi, amesema uboreshaji wa kiwanja hicho ulianza Septemba 2023 na unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 34, huku ukitarajiwa kukamilika Julai 2026.
Mhandisi Mweladzi amesema mradi huo unatekelezwa na China Railway Construction Engineering Group kwa gharama ya shilingi bilioni 51.4. Hadi sasa, mkandarasi amelipwa shilingi bilioni 24.5 kwa kazi zilizotekelezwa.
Ameeleza kuwa kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa maegesho ya ndege yenye uwezo wa kuhudumia ndege kubwa tisa aina ya Boeing 737 - 800 kwa wakati mmoja, tofauti na awali ambapo kiwanja hicho kilikuwa na uwezo wa kuhudumia ndege ndogo aina ya Bombardier Q400 pekee.
Kazi nyingine zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege (runway) yenye urefu wa kilomita 1.8, barabara za ndani zenye urefu wa kilomita 1.5, pamoja na maegesho ya magari yenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya magari 100 kwa wakati mmoja.
Aidha, Mkandarasi anaendelea na ujenzi wa jengo jipya la abiria litakalokuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 500 kwa wakati mmoja, jengo la kuongozea ndege, jengo la vifaa vya umeme vya taa za kuongozea ndege, na jengo la Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mweladzi, mradi huo ukikamilika utakuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Kigoma kwa kuimarisha usafiri wa anga katika ukanda wa magharibi mwa Tanzania na nchi jirani za Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mradi huo pia unatarajiwa kuongeza fursa za biashara na uwekezaji katika Mkoa wa Kigoma na maeneo mengine nchini.
Akimshukuru Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mhandisi Mweladzi amesema upatikanaji wa fedha za mradi umewezesha utekelezaji wake kuendelea bila changamoto za malipo kwa Mkandarasi.
"Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za mradi huu. Hadi sasa Mkandarasi hadai fedha yoyote, na matarajio yetu ni kuona mradi unakamilika kwa wakati na kwa viwango vya ubora vinavyotakiwa," amesema Mhandisi Mweladzi.
Naye Mhandisi Dadi Shahame kutoka Khatib & Alami Consulting Engineers Offshore amesema mkandarasi amewasilisha mpango kazi wa kufidia muda uliopotea.
Mpango huo unahusisha kuongeza saa za kazi, kuongeza idadi ya wafanyakazi na kushirikisha wakandarasi wadogo ili kuharakisha utekelezaji wa mradi katika kipindi kilichobaki.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

