EQUITY BENKI YAINGIA MAKUBALIANO NA TAASISI ZA KILIMO
BENKI ya biashara ya EQUITY imeingia makubaliano na taasisi mbili za kilimo na maendeleo ya jamii ya kutoa mikopo ya riba nafuu kwa wakulima wa mahindi mkoani Ruvuma.
Meneja Mkuu wa Biashara Benki ya Equity Leah Ayubu amesema hayo jijini Dodoma ambapo amesema kuwa benki hiyo imeingia makubaliano ya kiutendaji na taasisi za Private Agricultural Sector Support Trust (PASS) na Movement for Community Development Tanzania (MCODE).
Hata hivyo ameeleza kuwa lengo la makubaliano hayo yanalenga kuboresha maisha ya wakulima wadowadogo hususani waliopo vijijini.
“Wakulima walioko vijijini wanahitaji kufikishiwa huduma za kifedha kwa wingi hususani mikopo ya riba nafuu. Wamekuwa wakipata changamoto ya dhamana na hivyo makubaliano haya yanaenda kuondoa changamoto hiyo ya dhamana ambapo benki inachukua jukumu la kuwadhamini,” amesema Leah.
Hata hivyo ameeleza kuwa wakulima wanaohitaji mikopo watalipiwa hadi asilimia 80 ya dhamana wanazotakiwa kutoa ambapo mikopo itatolewa kwa wakulima wanaojihusisha na zao la chakula ya mahindi mkoani Ruvuma na mikoa ya nyanda za juu kusini.
Makubaliano hayo pia yatahusisha utoaji mafunzo kwa wakulima ya jinsi ya kuitumia mikopo kulingana na malengo yao ili waweze kukuza vipato na kurejesha mikopo hiyo kwa urahisi.
Sanjari na hayo amesema kuwa uwezeshaji wa benki hiyo unatoa kipaumbele kwa wanawake na vijana. Mwezi Mei mwaka huu benki hiyo ilizindua dirisha maalum la mikopo kwa wanawake kwa riba ya asilimia 15.
“Equity benki imekwisha toa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 20 hadi sasa tangu miaka mitatu iliyopita kwa wakulima wadogo,” ameeleza hayo Bi.Leah
Naye Meneja wa Kilimo wa benki hiyo, Theophola alisema MCODE inahudumia zaidi ya vikundi 1,000 vya wanawake mkoani Ruvuma na hivyo kuona ni taasisi muhimu ya kushirikiana nayo katika kuwafikia wakulima wadogo wa mahindi.
Aidha ameeleza kuwa taasis hiyo pia inahudumia wakulima katika mikoa ya Njombe, Rukwa, Songea, Mneya na Songwe. Wakulima waliofikiwa ni wenye eka moja hadi heka 10.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Biashara kutoka PASS Trust , Adam Kamanda alisema kuwa ubia huo ni wa uendelevu kibiashara kwa kutoa dhamana ya mikopo kwa wakulima wadogowadogo.
Amesema mikopo hiyo pia itawasaidia wakulima kupata mbegu na viuatilifu na kulima kisasa ili kuongeza tija ya mazao wanayozalisha.
“Tutaanza kwa kutoa mikopo kwa wakulima 30,000 ambapo tunalenga baada ya misimu kadhaa kuwafikia wakulima 100,000. Baada ya hapa tunaangalia uwezekano wa kuwafikia wakulima wanaojihusisha na mazao mengone ya chakula na biashara,” alisema Kamanda.
Wakizungumza baada ya kusaini mkataba huo viongozi wa taasisi hizo wameeleza lengo na ushirikiano huo.
Amesema PASS na benki ya Equity wanaushirikiano wa miaka mine hivi sasa katika kuwezesha makundi mengine ya jamii kiuchumi.
“Hadi Julai mwaka huu taasisi hiyo imekwisha dhamini mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 68 kwenye sekta za kilimo, uvuvi na mifugo.”
Naibu waziri wa kilimo David Silinde alishuhudia utiaji saini mkataba wa mashirikiano kati ya taasisi tatu ambozi ni EQUITY Benki ,taasisi ya biashara ya PASS na taasisi ya MCODE zenye lengo la kuboresha maisha ya watanzania hasa wakulima
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

