SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA UTAYARI WA KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MLIPUKO
Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola kwa kuendesha mafunzo kwa vitendo kwa wataalamu wa afya, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendelea kuimarisha uwezo wa mfumo wa afya katika kuzuia, kugundua na kutoa mwitikio wa haraka dhidi ya magonjwa ya mlipuko.
Hayo yamesemwa leo, Julai 17,2026, na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Sumbawanga, Dkt. Ismail Macha, wakati wa zoezi la usimamizi shirikishi na mafunzo kwa vitendo ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, amesema kuwa maandalizi ya kutosha ndiyo msingi wa kudhibiti athari za milipuko kwa wananchi.
“Ebola ni ugonjwa unaohitaji umakini mkubwa na hatua za haraka. Wataalamu wa afya wanapaswa kuwa na uwezo wa kutambua viashiria vya awali, kutoa taarifa kwa wakati na kuanzisha hatua za awali za udhibiti ili kuzuia kusambaa kwa maambukizi,” amesema Dkt. Macha.
Amesema usimamizi shirikisishi na mafunzo kwa vitendo hutoa nafasi ya kutathmini utendaji wa huduma za afya katika mazingira yanayofanana na hali halisi, jambo linalosaidia kubaini mapungufu yaliyopo na kuweka mikakati ya kuyafanyia kazi kabla ya kutokea kwa dharura.
Aidha, Dkt. Ismail Macha amesema mafanikio katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya wataalamu wa afya, viongozi wa sekta ya afya na taasisi mbalimbali, ili kuhakikisha kila ngazi inatimiza wajibu wake kwa wakati na kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Afisa Muuguzi kutoka Wizara ya Afya, Bi. Theresia Haule, amesema mafunzo hayo yanalenga kuendelea kujenga umahiri wa wataalamu wa afya katika kutoa huduma salama na kufuata taratibu za kitaalamu wakati wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, hatua inayochangia kuimarisha usalama wa wagonjwa na wahudumu wa afya.
Ameongeza kuwa Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuendesha mafunzo na usimamizi shirikishi katika maeneo mbalimbali nchini, kwa lengo la kuimarisha mfumo wa afya, kuongeza utayari wa kukabiliana na dharura za afya ya umma na kulinda afya za wananchi.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

