WATOTO WASHIRIKISHWE IPASAVYO KATIKA JAMII ILI KUELEZA CHANGAMOTO WANAZOZIPITIA -BARAZA LA WATOTO CHAMWINO
Kukithiri kwa mmomonyoko wa maadili katika jamii watoto waeleza namna ushirikishwaji duni kuanzia ngazi ya familia katika kutoa maamuzi kunavyoathiri ustawi wao.
Hayo yameelezwa na Baraza la Watoto kutoka halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika kijini cha kawawa Kata ya Msanga mikoani Dodoma yaliratibiwa na shirika la ACTION AID Tanzania.
Anthony Mlewa, mwenyekiti wa Baraza hilo amesema watoto hawashirikishwi ipasavyo kwa kuwapa muda kuueleza changamoto wanazozipitia hali inayojenga ukimya juu ya matukio ya ukatili wa kijinsia.
"Suala la ushirikishwaji duni kuanzia ngazi ya familia hasa katika mambo ya kutoa maamuzi Bado ni janga kwetu, tushirikishwe", alisema Mlewa.
Nae, Makamu mwenyekiti wa Baraza, Jackline Peter, amesema juu ya ushiriki wa wanajamii katika kutokomeza matendo ukatili kwa watoto akiwarai wazazi kutokuwalaza watoto na wageni.
"Wanaofanya ukatili zaidi ni ndugu wa karibu tuchukue tahadhali ikiwemo kutowachanganya watoto na wageni, tusiwachukulie wageni poa Wala kuwaamini", alisema.
Kwa upande wake Afisa ustawi wa Jamii, Abed Fred, kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, amebainisha moja ya changamoto iliyoko kwenye jamii ni ushiriki hafifu wa wazazi katika malezi ya watoto.
“Jukumu la kulea hawa watoto ili waweze kuwa na maadili na stadi nzuri za kazi ni letu sisi wazazi, ukisikia mmomonyoko wa maadili chanzo ni sisi, inategemea na kile ambacho mtoto anakipata kwetu.
“Kumekuwa na tabia ya wazazi ya sisi kina baba na kinamama, mtoto akitoka shule badala ya kuzungumza nae kwa upendo na kumfundisha maadili, mnampa mtoto simu achezee ili asiwasumbue, muendelee na mambo yenu, unajua mtoto anafungua nini humo? changamoto huanzia hapo”, alisema Fred.
Janeth Nyamayahasi, ambaye nimwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Wakulima Wilaya ya Chamwino, pamojana Clesencia Sahani ambaye ni mwakilishi wa shirika hilo wakieleza bayana hali halisi ya mtindo wa maisha wa sasa unavyowalazimu kuwa mbali na malezi ya watoto.
“Tunasema watoto wanajifunza wapi? Lakini kumbe ni nyumbani kwa wazazi watoto, kuna wakati sisi tunasababisha, hasa katika maswala ya utandawazi watoto wanajifunza, tuhakikishe wanachojifunza kiendeane na maadili na utamaduni wetu", alisema Sahani.
“Wazazi tumekuwa busy mno na shughuli za uzalishaji, lishe na kukimbizana na marejesho, tunashindwa kuangalia watoto wako wapi, hata nyakati za jioni tunaporudi watoto hatuwatilii maanani, tuko busy na uchovu, tunajikuta watoto wanakuwa kwa jirani au vibanda bubu kuangalia TV hatujui kipindi cha usiku kinachooneshwa kule ni nini", alisema Nyamayahasi.
Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto Wilaya ya Chamwino MRAKIBU MSAIDIZI WA POLISI (ASP), YUSUPH ABDALLAH, amebainishwa umuhimu wa wazazi wa kutenga muda wa kuongea na watoto.
“Mtoto ameenda shule anarudi huna hata muda hata wa robo au nusu saa wa kuzungumza nae, ukamuhoji, umesoma nini, umekutana na nini ama una changamoto gani.
“Hatuna ukaribu na watoto, sisi wazazi tujitahidi kuwa nao karibu, wana mambo mengi hwawa, sisi huwa tunazunguka mashuleni kuzungumza nao, mambo mengine wanayotueleza ni ya aibu kabisa na ya kusikitisha”, alisema ASP Abdallah
ASP Abdallah amebainisha kuwa Jumla ya kesi 118 za ukatili wa kijinsia zilifunguliwa Wilaya ya Chamwino katika kipindi cha Oktoba 2023 hadi Juni 2024, kesi 109 kati ya hizo walitendewa jinsi ya kike na kesi 9 walitendewa jinsi ya kiume.
Maadhimisho hayo yalienda sambamba na burudani na michezo mbalimbali kutoka kwa wanafunzi yakienda sambamba na kauli isemayo "Elimu jumuishi kwa watoto izingatie maarifa, maadili na stadi za Kazi".
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

