NELSON MANDELA MWENYEJI MASHINDANO YA FEAUS 2024
Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela mwenyeji wa Michuano ya tatu Shirikisho la Michezo ya Vyuo Vikuu Afrika Mashariki (FEAUS), yaliyoanza tarehe 28 - 30 Machi 2024 na yakihusisha wanamichezo wanawake kwa mwaka huu.
Michuano hiyo imefunguliwa Machi 28, 2024 katika Taasisi hiyo kwa mdahalo maalumu wa kijinsia na kuangalia vikwazo au changamoto wanazopitia wanafunzi wa kike katika kushiriki michezo ya vyuo vikuu.
Mkurugenzi wa Tafiti na Ubunifu kutoka taasisi hiyo,Pof.Revocatus Machunda akimwakilisha Makamu Mkuu wa Taasisi amesema taasisi hiyo imekuwa ikiunga mkono michezo kwa wanafunzi na wafanyakazi ili kuwa na afya njema pamoja na kufanya vizuri katika tafiti na ubunifu.
Amesema kama ilivyo katika masomo ya Sayansi hivyo hivyo taasisi inaweka mazingira wezeshi kwa wanawake, wasichana na watu wenye mahitaji maalumu kushiriki katika michezo ikiwemo miundombinu.
Kwa upande wake rais wa FEAUS Prof. Simon Munai amesema lengo kuu ni kuhamasisha ushiriki wa wanavyuo wa jinsia ya kike katika michezo, pia michezo ni muhimu kwani ni mojawapo ya njia ya kupata ajira na vilevile huimarisha afya ya mwili.
Amezisisitiza jamii za waafrika kuwapa wanawake uhuru na nafasi ya kushiriki michezo na kuacha mila potofu juu ya ushiriki wa wanawake katika michezo.
Naye,Bw.Noel Kiunsi Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la michezo ya Vyuo Vikuu Tanzania ambaye pia ni mkufunzi mkuu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam,ameongeza kuwa michezo hiyo kwa wanavyuo inatoa fursa ya kuwakutanisha wanafunzi kutoka nchi na vyuo tofauti ili kubadilishana uzoefu.
Vilevile Diana Barasa mwanafunzi wa Shahada ya kwanza ya watoto wenye mahitaji maalumu kutoka nchini Kenya amesema michezo inawahamasisha wadau hao kuwapa kipaumbele wanawake na kuzishabikia timu za wanawake kama ilivyo kwa wanaume.
Mashindano hayo yatafanyika katika viwanja vya michezo vya Taasisi ya Nelson Mandela.
#JordanMediaupdates
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

