TANROADS YAKANUSHA BARABARA KUJENGWA CHINI YA KIWANGO
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma umekanusha taarifa inayosambaa katika mitandao ya kijamii ikionesha kipande cha barabara kilichojengwa chini ya kiwango katika eneo la Makaravati Wilayani Kongwa katika barabara kuu ya Dodoma - Gairo.
Taarifa sahihi ni kuwa kipande cha barabara hiyo ni sehemu ya majaribio iliyojengwa kwa mujibu wa taratibu za kitaalamu kabla ya ujenzi kamili kuanza.
Akizungumza mkoani Dodoma, Mhandisi Mkazi wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Elisony Mweladzi, amesema kipande hicho chenye urefu wa mita 300 kilijengwa mahsusi kwa ajili ya majaribio kabla ya kuwekwa tabaka la mwisho la lami hatua ambayo ni ya kawaida katika miradi ya ujenzi wa barabara.
“Kwa kawaida kabla ya kuweka lami, huwa unaweka eneo la majaribio kwa hiyo Mkandarasi anapewa eneo ya mita 300 kwa ajili ya majaribio kuona kama vipimo vyote vya lami vinakidhi viwango”, amesema Mhandisi Elisony.
Amesema baada ya kipande hicho kupimwa na maabara ya TANROADS, ilibainika kuwa hakikukidhi viwango vilivyokubaliwa, jambo lililosababisha Mamlaka hiyo kumwandikia barua Mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuanza mara moja kufanya marekebisho ya mapungufu yaliyojitokeza ikiwemo kukiondoa kwa gharama zake.
Mhandisi Elisony amesisitiza kuwa TANROADS itaendelea kumsimamia kwa karibu Mkandarasi ili kuhakikisha ujenzi unazingatia viwango na thamani ya fedha za umma.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka kwa Mkandarasi Kings Builders anayetekeleza ujenzi wa mradi huo, Edward Njau amekiri kupokea barua kutoka TANROADS kwa ajili ya kufanya marekebisho, na ameahidi kutekeleza maelekezo hayo mara moja.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

