RAIS SAMIA ATOA MSAMAHA KWA WAFUNGWA 1,036 MIAKA 64 YA UHURU
Wakati Tanzania Bara inaadhimisha miaka 64 ya Uhuru, Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza msamaha kwa jumla ya wafungwa 1,036, ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa kila mwaka wa kuadhimisha siku hiyo muhimu.
Kati ya walioguswa na msamaha huo, wafungwa 22 wameachiwa huru kabisa, huku 1,014 wakipunguziwa adhabu na hivyo kuendelea kutumikia vifungo vilivyobaki gerezani.
Idadi ya walioachiwa huru mwaka huu, Desemba 9, 2025, inafanana na ile ya mwaka jana katika sherehe kama hizo.
Msamaha huu unatolewa chini ya mamlaka ya Rais kupitia Ibara ya 45(1)(a)-(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa rasmi juu ya msamaha huo imetolewa leo na Wizara ya Mambo ya Ndani, kupitia hati iliyosainiwa na Waziri wa Wizara hiyo, George Simbachawene, ambaye ameongeza kuwa Serikali inatarajia wale walioachiwa huru watadumisha maadili mema na kuacha tabia zinazoweza kuwarudisha gerezani.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

