logo

DKT.BITEKO AZINDUA KIWANDA CHA KUWEKA MIFUMO YA UPASHAJI NA UTUNZAJI JOTO MABOMBA YA EACOP

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt.Doto Biteko amezindua Kiwanda cha kuwekea mifumo ya kupasha na kutunza joto katika mabomba yatakayosafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga nchini Tanzania kupitia Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

Akizindua mradi huo katika Kijiji cha Sojo wilayani Nzega mkoani Tabora, Dkt.Biteko amesema utekelezaji wa mradi wa EACOP umefikia asilimia 27 ikiwa ni kielelezo cha usimamizi madhubuti wa Rais wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda, Mhe.Yoweri Kaguta Museveni ambao wamekuwa vinara katika kuhakikisha mradi unafanyika kwa wakati na viwango vya kimataifa.

Amesema Rais Samia amesimamia kikamilifu mradi kutoka alipoupokea mwaka 2021 kwa kuhakikisha Serikali inatekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwemo kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huo kwa wakati ambapo hadi sasa Serikali imetoa jumla ya shilingi Bilioni 710 kati ya shilingi Bilioni 820 sawa na asilimia 87 ikiwa ni mchango wake kama Mwanahisa katika mradi wa EACOP.

Amesema utekelezaji wa mradi huo unaendelea vizuri ikiwemo suala la utwaaji wa ardhi ambapo malipo yamefanyika kwa asilimia 99.2, ujenzi wa matenki makubwa ya kuhifadhi mafuta Chongoleani Tanga umeshaanza na kufikia asilimia 32 na gati ya kupakia mafuta katika eneo la Chongoleani umefikia asilimia 36.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameitaka kampuni ya EACOP kuhakikisha inatoa kipaumbele zaidi kwa watanzania katika fursa mbalimbali na kutoa onyo kwa kampuni za nje ambazo zinachukua fursa za Watanzania kwa kujifanya ni kampuni za ndani ya nchi ambapo udanganyifu huo wamekuwa wakiufanya kwa kushirikiana na baadhi ya watanzania.

"Kumeanza kutokea mchezo kwa baadhi ya kampuni za nje kwa kushirikiana na baadhi ya Watanzania wanatengeneza kampuni ionekane ni ya kitanzania, tumefanya kazi ya kuzikagua kampuni hizi kwa kutumia EWURA na zile zilizobainika zmefanya udanganyifu tumezifuta ili kampuni za ndani zipate kazi kwanza, fursa hizi zinapokuja lazima ziwafaidishe Watanzania kwanza, kampuni zinazotoa huduma lazima ziwe za kitanzania na hii ni kwa mujibu wa sheria ya nchi." Amesema Dkt. Biteko

Vilevile ameitaka kampuni ya EACOP kushirikisha wananchi wanaozunguka mradi huo ili wawe ni sehemu ya mradi na kuwa Walinzi wa mradi husika na kuangalia namna bora ya kuwawezesha ili hata baada ya ujenzi wa mradi kukamilika wananchi wa jamii hizo waendelee na shughuli zao (sustainability empowerment)

Amesema Tabora ipo eneo la katikati la utekelezaji wa mradi huo wenye urefu wa kilometa 1443 hivyo waone mradi huo ni wao na watoe ushirikiano kwa wakandarasi na Serikali kwa upande wake itahakikisha wanapata yale yote wanayostahili kutokana na uwepo wa mradi huo ikiwemo huduma za kijamii na fursa za mradi.

Vilevile ametoa pongezi kwa Serikali ya Uganda kwa kuiona Tanzania kama mdau muhimu kwenye maedeleo ya nchi yao na kwamba Serikali ya Tanzania inatambua mchango huo na kuuthamini.

Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali ya Tanzania na Uganda zipo kwenye majadiliano ya kutekeleza mradi mwingine mkubwa wa Bomba la Gesi kutoka Tanzania kwenda Uganda ikiwa ni maelekezo ya viongozi Wakuu wa Nchi hivyo Wizara ya Nishati itayasimamia kikamilifu.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa Rais Samia anataka kuwaletea maendeleo Watanzania wote, kuwatoa kwenye umaskini na kuwainua kiuchumi kwa kushirikiana na Sekta binafsi hivyo ni muhimu kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Sekta binafsi na kutowakwamisha.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Mhe. Ruth Nankabirwa amesema kuwa, uzinduzi wa kiwanda hicho ni kielelezo cha hatua kubwa iliyopigwa kwenye utekelezaji wa mradi ambapo ameipongeza kampuni ya EACOP kwa mradi huo ambao umezingatia viwango vya kitaifa na kimataifa vya utekelezaji wa miradi ikiwemo za utunzaji wa mazingira.

Amesema Serikali ya Uganda inaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania ili kutekeleza mradi huo kwa ufanisi na kwa wakati.

Aidha, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Uganda katika nyanja mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa mradi huo wa EACOP.

Ameongeza kuwa shughuli za utafiti na uchimbaji wa mafuta nchini Uganda zinaendelea vizuri hali inayoendelea kutoa uhakika katika utekelezaji wa mradi wa EACOP.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato amesema kuwa mradi wa EACOP ulikumbwa na changamoto katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn