KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ELIMU YATEMBELEA TAASISI YA NELSON MANDELA
Kamati ya Kudumu ya Bunge, Elimu, Utamaduni na Michezo imetembelea Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela(NM-AIST) kwa ajili ya kujionea mradi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 16.28.
Mradi huo wa ujenzi wa bweni utaweza kutoa fursa kwa wanawake wenye watoto wachanga wanaofika kusoma na kufanya tafiti mbalimbali zenye matokeo chanya kwa wananchi, kilimo sanjari na sekta nyingine za kuinua uchumi wa kati.
Hayo yamesemwa Machi 12,2024 jijini Arusha na Makamu Mkuu wa Taasisi , Profesa Maulililo Kipanyula mbele ya kamati hiyo wakati akielezea hatua mbalimbali za ujenzi wa mabweni hayo yatakayokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 500 mara yatakapokamilika.
Profesa Kipanyula amesema ujenzi huo unatekelezwa kwa awamu tatu lengo ni kuongeza fursa kwa wanawake kushiriki katika masuala ya sayansi, teknolojia, ubunifu ambapo mpango wa ujenzi huo ni wa miaka mitano.
Amesema ujenzi wa mabweni hayo umewekwa katika awamu tatu ambapo kila awamu itagharimu kiasi cha shilingi bilioni 5.8 na awamu ya kwanza katika ujenzi unaoendelea bajeti yake ni shilingi bilioni 5.8 huku lengo la mradi huo likiwa ni kutengeneza fursa kwa wanawake na kuongeza kuwa ujenzi wa bweni hilo umefikia asilimia 49.
"Mabweni haya yapo katika mfumo wa nyumba zenye vyumba viwili vinavyomuwezesha mwanamke anayenyonyesha kupata nafasi ya kusoma na kuishi na familia yake, pia kutoa nafasi zaidi kwa wanawake kupenda zaidi masomo ya sayansi. Mwaka ujao wa fedha tutakamilisha ujenzi huo kwa asilimia 100",alisema Profesa Kipanyula.
Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga ameishukuru kamati hiyo kwa kutembelea ujenzi huo wa mabweni uliotengewa fedha mwaka 2023/24 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi zaidi ya 500.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Husna Sekiboko amesema wajumbe wa kamati hiyo wametembelea eneo la mradi kujionea uhalisia wa fedha zilizotumika na wanaamini hivi sasa mradi huo wa bweni utaenda kasi kwa kuwa serikali imeshatoa fedha na kwenye bajeti ya mwaka huu wataendelea kutenga fedha nyingi zaidi ili ndoto za wanawake katika masuala ya sayansi ziweze kutimia.
#JordanMediaupdates
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

