logo

WAZIRI MKENDA: WATAKAOIBA MITIHANI TUTAWASHTAKI, KANUNI NA TARATIBU ZIFUATWE

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.Prof.Adolf Mkenda amewataka wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani yao ya kumaliza elimu ya msingi kufuata kanuni na taratibu za mitihani, na kwa wale wachache wenye msukumo wa kufanya udanganyifu wasifanye hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

.

"Wanafunzi wajue unapofanya udanganyifu kwenye chumba cha mtihani au kuandika maneno yasiyo faa kwenye karatasi za kujibia mtihani matokeo yako yanafutwa na madhara yake yanakuwa ni makubwa Sana" amesema Mkenda.

.

Mkenda ameyasema hayo leo Septemba 12,2023 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma mara baada ya Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania(NECTA) kutoa taarifa ya mitihani ya darasa la Saba ambayo itaanza kufanyika kesho tarehe 13 mwezi Septemba 2023 Hadi tarehe 14 mwezi Septemba 2023 Tanzania nzima.

.

Amesema suala la wizi katika mtihani wanaendelea kulikemea na kwa hivi sasa hali imekuwa nzuri sana, mtihani uliopita waliona kwamba ngazi ya udanganyifu iliyokuwa ikifanyika umetoweka kwa hivi sasa kutokana na hatua kali walizozichukua na wanatarajia hali hiyo itaeendelea.

.

Waziri huyo amehimiza watu wote hasa maafisa wa serikali, maafisa elimu na kamati za mitihani kuanzia shuleni mpaka mikoani wahakikishe hakuna wizi wa mitihani.

.

"Popote pale awe afisa wa serikali au mwalimu atakayebainika kujihusisha kwa namna yoyote na udanganyifu wa mitihani tutahakikisha anafukuzwa kazi na atashtakiwa" amesema Mkenda.

.

Aidha, Mkenda amesema Baraza la Mitihani la Tanzania limetoa namba kwa mtu yeyote atakayeona vitendo vya wizi wa mitihani vinafanyika atoe taarifa kwa siri kupitia namba 0759360000.

.

Jumla ya watahiniwa waliosajiliwa 1,397,370 ambapo kati yao wavulana 654,652 sawa na asilimia 46.85 na wasichana 742,718 sawa na asilimia 53.15 watafanya mtihani huo.

#JordanMediaupdates

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn