logo

TARURA TUNAKWENDA KUJENGA KILOMITA 427 KWA KIWANGO CHA LAMI

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi.Victor Seff amesema katika mwaka wa fedha 2023/24, jumla ya barabara zenye urefu wa kilomita 21,057.06 zitafanyiwa matengenezo, kilomita 427 zitajengwa kwa kiwango cha lami, km 8,775.62 zitajengwa kwa kiwango cha changarawe, madaraja na makalavati 855 yatajengwa pamoja na mifereji ya mvua km 70.

.

Mhandisi Seff amesema hayo leo Agosti 24,2023 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa majukumu ya wakala hiyo na mwelekeo wake katika mwaka wa fedha 2023/24 katika ukumbi wa Idara Ya Habari Maelezo Jijini Dodoma.

.

Amesema mojawapo ya kipaumbele cha TARURA ni kutumia malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi ili kupata ufanisi wa gharama za ujenzi, hadi Mwezi Machi, 2023 TARURA imejenga madaraja 163 ya mawe yenye thamani ya shilingi bilioni 8.7 ambapo gharama imepungua kwa zaidi ya asilimia 50.

.

"Madaraja hayo yamejengwa katika mikoa ya Kigoma 92, Singida 24, Tabora 5, Kilimanjaro 10, Mbeya 2, Arusha 6, Morogoro 2, Rukwa 3, Pwani 1, Ruvuma 3 na Iringa 15" amesema Seff.

.

Mtendaji Mkuu huyo amesema jumla ya shilingi Bilioni 858.517 zimeidhinishwa kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya barabara za Wilaya. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 710.31 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 148.207 ni fedha za nje kupitia miradi ya RISE, TACTIC, Bonde la mto Msimbazi na Mradi wa Agri connect.

.

Aidha, Seff amesema kupitia fedha za ndani, jumla ya kilomita 22,523.51 zimefanyiwa matengenezo (utunzaji wa barabara), ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kilomita 249.74, ujenzi wa barabara kwa changarawe kilomita 9,761.01, ujenzi wa madaraja na makalavati 463 pamoja na ujenzi wa mifereji ya kuondoa maji barabarani kilomita 64.47.

.

Naye Msemaji Mkuu wa Serikali Ndg.Gerson Msigwa amesema watanzania wana kila sababu ya kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuhakikisha taasisi zote za Serikali zinazofanya biashara na zisizofanya biashara zinafanya kazi zake kwa tija.

#JordanMediaupdates

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn