logo

WAZIRI MKENDA ATAKA VYUO VIKUU KUONA UMUHIMU WA KUIMARISHA UBORA WA ELIMU

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ametoa wito kwa Vyuo Vikuu nchini kuona umuhimu wa kuimarisha ubora wa elimu ya juu ili iweze kuakisi mahitaji ya nchi, soko la ajira kikanda na kimataifa.

Mkenda ametoa wito huo Jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga warsha ya kubadilishana uzoefu kwa Wenyeviti na Wajumbe wa Mabaraza, Seneti na Bodi za Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki ambapo amesema lengo ni kuwa na wahitimu bora.

Pia amevishauri Vyuo kuona ni namna gani wanaweka viwango vinavyofanana vya ubora kwa vyuo Vikuu vyote na kwamba kama hilo lisipofanikiwa kuwepo na gredi ambazo zitakuwa zikitumiwa na Vyuo Vikuu.

“Kuweka viwango itasaidia mhitimu wa Chuo A asionekane ni tofauti na wa Chuo B ili wawe na nafasi sawa za ajira. Msukumo mkubwa wa Vyuo ni kuwa na wanafunzi wengi, ninawaomba _tusicompromise_ ubora wa elimu,”amesema Mkenda

Ameongeza kuwa kazi ya Vyuo Vikuu ni kuzalisha na kusambaza uelewa hivyo wahadhiri wa Vyuo vikuu lazima wawe wanafanya kazi za tafiti ili kutafuta ugunduzi mbalimbali wakati wanafundisha.

“Vyuo ni lazima viendele kujenga mazingira mazuri ya wahadhiri wake kufanya utafiti vipo baadhi ya Vyuo ambavyo inaonekana mtizamo wake ni kama utafiti ni chanzo cha mapato haiwezi kuwa hivyo na haitakiwi kuwa hivyo utafiti ni chanzo cha maarifa kwa hiyo lengo la utafiti kwa vyuo vikuu ni kuwa na maarifa mapya,” amesisitiza Mkenda.

Akizungumzia mageuzi ya elimu yanayofanyika nchini Prof Mkenda amevitaka Vyuo Vikuu kuona umuhimu wa kuandaa walimu kwa ajili ya kufundisha katika mkondo wa Elimu ya Amali. Lengo ni shule za Ufundi zitakapoanza kutoa elimu ya ufundi kuwe na walimu waliosoma ualimu lakini wamesomea na mafunzo ya Amali mfano Uhandisi na Kilimo.

"Kuelekea kwenye kufufua shule zetu za ufundi ni lazima tuandae walimu kwa ajili ya kwenda kufundisha mafunzo ya Amali hivyo vyuo vinavyotoa Kozi ya ualimu waongeza na mafunzo ya Amali kwa mfano Chuo Kikuu Cha Sokoine wanatoa Ualimu na Kilimo hivyo tayari mwalimu akimaliza anaweza kufunduasha Mafunzo ya Amali," ameeleza Mkenda.

@wizara_elimutanzania

#JordanMediaupdates

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn