JUKWAA LA MAFUTA YA KULA LAZINDULIWA DODOMA
Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), amezindua rasmi Jukwaa la Uwekezaji na Uwezeshaji wa Tasnia ya Mafuta ya Kula jijini Dodoma, akihimiza ongezeko la uwekezaji katika uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta ili kuiwezesha Tanzania kujitosheleza kwa mafuta ya kula na kushindana katika masoko ya kimataifa.
.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Chongolo amezitaka taasisi za fedha kubuni mifumo ya mikopo ya muda mrefu inayokidhi mahitaji ya wakulima na wawekezaji katika sekta ya mbegu za mafuta, hatua itakayochochea uzalishaji na ukuaji wa tasnia hiyo.
.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kubadili mtazamo kutoka kwenye uchuuzi na kuelekea kwenye uzalishaji wenye tija, akibainisha kuwa Tanzania ina ardhi ya kutosha na Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, uzalishaji na biashara ya mafuta ya kula.
.
Jukwaa hilo limeandaliwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda na Biashara, huku COPRA ikiratibu maandalizi ya Mkakati wa Taifa wa Mafuta ya Kula wa mwaka 2026–2035 pamoja na kusimamia utekelezaji wa Kanuni za Usimamizi wa Mafuta ya Kula.
.
Mhe. Chongolo pia ameipongeza timu ya wataalamu iliyoongozwa na Bw. Charles Ogutu kwa kazi ya kuandaa mkakati huo, akieleza kuwa upo katika hatua za mwisho za kukamilishwa.
.
Amesema mafanikio ya sekta ya mafuta ya kula yatategemea ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha na wadau wengine katika kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya mbegu za mafuta.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

