NEMC YAADHIMISHA MIAKA 40 KWA UZINDUZI WA TOCEMS JIJINI DAR
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amezindua Mfumo wa Kidigitali wa Kufuatilia Uchafuzi wa Mazingira (TOCEMS) wakati wa Kongamano la Kisayansi la Maadhimisho ya Miaka 40 ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
.
Katika hafla hiyo, Dkt. Nchemba alimpongeza NEMC kwa juhudi kubwa na mafanikio ya miongo minne katika Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini.
Kongamano hilo lilifanyika Mei 28, 2026, katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, likiwa na kaulimbiu “NEMC@40: Tunza Mazingira, Linda Taifa.”
.
Lengo kuu lilikuwa kujadili mchango wa usimamizi wa mazingira katika maendeleo endelevu ya Taifa pamoja na kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali za kimazingira zinazoikabili nchi.
Akizungumza na wajumbe, Dkt. Nchemba alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano na NEMC ili kuhakikisha sheria, kanuni na miongozo ya mazingira inatekelezwa ipasavyo katika sekta zote za maendeleo.
.
Alibainisha kuwa uhifadhi wa mazingira si jukumu la taasisi moja pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi na kila sekta kwa mustakabali wa Taifa na vizazi vijavyo.
Aidha, Serikali inaendelea kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kudhibiti shughuli zinazosababisha uharibifu wa mazingira.
Mfumo wa TOSEMS uliozinduliwa unalenga kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli zinazoweza kusababisha uchafuzi wa mazingira nchini.
.
Dkt. Nchemba alieleza kuwa mfumo huo utaongeza ufanisi katika ukusanyaji wa taarifa, ufuatiliaji wa viashiria vya uchafuzi na kurahisisha utoaji wa taarifa kwa mamlaka husika ili kuchukua hatua za haraka. Hatua hiyo inatarajiwa kuboresha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa mazingira.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, aliahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha rasilimali za Taifa zinalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

