logo

RC SENYAMULE AHAMASISHA MCHANGO WA MFUKO WA UPANDIKIZAJI ULOTO NA FIGO BMH

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ametoa wito kwa wananchi, taasisi na wadau wa afya kushiriki kuchangia Mfuko wa Upandikizaji Uloto na Figo wa Benjamin Mkapa Hospital ili kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji wa huduma hizo muhimu za kibingwa.

‎Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mhe. Senyamule amesema gharama za huduma za upandikizaji figo na uloto bado ni kubwa kwa wagonjwa wengi, jambo linaloonesha umuhimu wa ushiriki wa jamii na wadau mbalimbali katika kusaidia wagonjwa kupata huduma hizo kwa wakati.

‎Amesema Benjamin Mkapa Hospital imeendelea kuwa nguzo muhimu ya huduma za afya za kibingwa nchini kwa kufanikisha matibabu ya upandikizaji ambayo hapo awali yalihitaji wagonjwa wengi kusafiri nje ya Tanzania.

‎“Zaidi ya wagonjwa 55 wamepatiwa huduma ya upandikizaji figo nchini, huku watoto 28 wakifanyiwa upandikizaji uloto. Haya ni mafanikio makubwa yanayoonesha uwezo wa wataalamu wetu wa ndani,” alisema Mhe. Senyamule.

‎Aidha, amesema bado zipo changamoto za kifedha zinazowazuia baadhi ya wagonjwa kupata huduma hizo muhimu, hivyo kuwataka wananchi na wadau mbalimbali kuunga mkono mfuko huo ili kuwafikia wagonjwa wengi zaidi.

‎“Kila mchango una nafasi ya kuokoa maisha ya mgonjwa anayehitaji huduma hizi. Tunahitaji ushirikiano mpana kuhakikisha wagonjwa wengi zaidi wanafikiwa,” alisisitiza.

‎Mhe. Senyamule ameongeza kuwa Mkoa wa Dodoma utaendelea kushirikiana na Benjamin Mkapa Hospital katika programu mbalimbali za kuhamasisha Watanzania na wadau kushiriki kuchangia Mfuko wa Upandikizaji Uloto na Figo.

‎Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Benjamin Mkapa Hospital, Dk. Henry Humba amesema mfuko huo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya hospitali hiyo tangu kuanzishwa kwake, ukiwa na lengo la kuongeza ushiriki wa jamii katika kuimarisha huduma za afya za kibingwa nchini.

‎Dk. Humba pia ameeleza kuwa kutokana na mguso wa kipekee wa Samia Suluhu Hassan, Serikali imewezesha upatikanaji wa takribani shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kusaidia wagonjwa.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn