MFUNGWA ALIYEMALIZA KIFUNGO AKABIDHIWA VIFAA VYA UJENZI MAGEREZA NJOMBE
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Njombe, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Joseph Michael Mkude, Aprili 2, 2026, kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Magereza Tanzania, CGP Jeremiah Yoram Katungu, amemkabidhi vifaa vya ujenzi Rashid Salehe Shemndorwa, mfungwa aliyemaliza kifungo chake mkoani Njombe.
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, ACP Mkude amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Mkuu wa Jeshi la Magereza wakati wa ziara yake mkoani humo.
.
Ameeleza kuwa Shemndorwa ni miongoni mwa wafungwa waliopata mafunzo ya ufundi wakiwa gerezani kupitia Chuo cha Magereza Ruanda kilichopo mkoani Mbeya.
“Leo tunamkabidhi vifaa hivi ndugu yetu Shemndorwa baada ya kumaliza kifungo chake. Hii ni ahadi ya Mkuu wetu wa Jeshi. Huu ndio urekebishaji wa kweli; tumempa ujuzi na sasa tunampa vifaa ili akautumie kujipatia kipato halali,” alisema ACP Mkude.
Kwa upande wake, Rashid Salehe Shemndorwa, mzaliwa wa Tanga, amelishukuru Jeshi la Magereza kwa kumpatia fursa ya kupata ujuzi akiwa gerezani.
.
Amesema nidhamu na kujituma katika kazi alizopangiwa kila siku zilimsaidia kufikia hatua hiyo.
Shemndorwa amesema baada ya kutoka gerezani ana mpango wa kuendeleza shughuli za ujenzi mkoani Tanga, huku akiahidi kuwa raia mwema na balozi mzuri wa Jeshi la Magereza kupitia ujuzi alioupata.
Pia ametoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kuwanyanyapaa watu wanaotoka magerezani, badala yake kuwapa ushirikiano ili wasirudi kwenye uhalifu.
“Natoa shukrani za dhati kwa Jeshi la Magereza kwa kunipa ujuzi ambao sikuwa nao. Vifaa hivi vitanisaidia kuanza maisha mapya na kuihudumia familia yangu kwa njia halali,” alisema Shemndorwa.
Rashid Shemndorwa alitumikia kifungo cha miaka 15 gerezani, ambapo amesema amejifunza mambo mengi ikiwemo kuishi vizuri na jamii.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

