logo

ZAIDI YA MALALAMIKO 2,000 YAPOKELEWA KUPITIA KITUO CHA HUDUMA-DKT.HOMERA

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, leo tarehe 17 Machi,2026 amezindua rasmi programu ya 'Sema Na Waziri' inayolenga kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi moja kwa moja.

‎Uzinduzi huo umefanyika katika ofisi za Wizara Mtumba jijini Dodoma, ambapo wananchi wataweza kuwasiliana kupitia Kituo cha Huduma kwa Mteja kwa namba 026 2160 360 au 0800 004 044.

‎Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Dkt. Homera amesema programu hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yanayosisitiza umuhimu wa Serikali kusikiliza na kutatua kero za wananchi, hasa zinazohusiana na masuala ya kisheria.

‎Ameeleza kuwa kituo hicho kilianzishwa Februari 14, 2024, lakini kuanzishwa kwa programu ya “Sema na Waziri” ni hatua ya kuboresha zaidi utoaji wa huduma kwa wananchi kote nchini.

‎Kwa mujibu wa Waziri Dkt. Homera, programu hiyo itakuwa inafanyika kati ya mara mbili hadi tatu kwa mwezi, ambapo Waziri atakuwa anazungumza moja kwa moja na wananchi ili kusikiliza na kutoa mwongozo wa changamoto zao.

‎"Tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Huduma kwa Mteja, jumla ya malalamiko 2,023 yamepokelewa, yakihusisha masuala ya ardhi, ndoa na talaka, ajira, mirathi, ukatili wa kijinsia pamoja na matunzo ya watoto. Kati ya hayo, malalamiko 1,394 yamepatiwa ufafanuzi huku 481 yakiendelea kushughulikiwa" alisema Dkt. Homera.

‎Aidha, Dkt. Homera amesisitiza kuwa programu hiyo pia inalenga kupunguza adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma, kwa kuwa sasa wanaweza kupata msaada wa kisheria kwa urahisi zaidi.

‎.

‎“Dhamira yetu ni kusikiliza kila mwananchi na kumwelekeza namna ya kupata haki yake bila kujali aina ya changamoto aliyonayo.” alisema Dkt.Homera.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn