logo

SERIKALI YATENGA BILIONI 32.25 KUIMARISHA MAABARA TANZANIA

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imesema imefanikiwa kufanya uchunguzi wa kisayansi wa vielelezo na sampuli 247,286 katika kipindi cha Januari 2025 hadi Februari 2026, hatua inayochochewa na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi pamoja na kuimarika kwa ubora wa huduma za maabara zinazotolewa na mamlaka hiyo.

‎.

‎Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dodoma, Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko, amesema mafanikio hayo pia yametokana na ushirikiano mzuri kati ya mamlaka hiyo na taasisi mbalimbali za serikali na wadau wa sekta ya afya.

‎.

‎"Taasisi hizo ni pamoja na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Jeshi la Polisi Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), pamoja na wadau wengine wa afya kama hospitali, Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)" alisema Dkt.Mafumiko.

‎.

Dkt. Mafumiko ameeleza kuwa huduma za uchunguzi wa kimaabara zimekuwa na mchango mkubwa kwa jamii, hususan kwa vijana, kwa kusaidia kudhibiti dawa za kulevya na kupunguza athari zake kwa jamii.

‎.

‎Aidha, uchunguzi huo unahakikisha ubora na usalama wa dawa asili zinazozalishwa na wataalamu mbalimbali wakiwemo vijana, hali inayochochea ajira na kujiajiri.

‎.

‎Kwa upande wa miundombinu ya maabara, amesema Mamlaka hiyo imefanikiwa kuwekeza katika mitambo mikubwa ya kisasa 32 na vifaa vidogo 542 kwa ajili ya kuboresha huduma za uchunguzi wa kisayansi.

‎.

‎"Uwekezaji huo wenye thamani ya Shilingi bilioni 32.25 umewezeshwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, mbali na hilo, mamlaka imetoa vibali 29,314 vya kuingiza shehena za kemikali nchini katika kipindi hicho.

‎.

‎"Kila shehena inapogombolewa kwa kufuata taratibu za forodha, shughuli ambayo kwa kiasi kikubwa hufanywa na vijana, hivyo kutoa fursa za ajira kwa wananchi na wadau wanaojihusisha na ugomboaji katika bandari na mipakani" alisema.

‎Katika sekta ya usafirishaji wa kemikali,Dkt. Mafumiko,amesema mamlaka hiyo ilitoa vibali vya kusafirisha takribani tani 1,829,825 za kemikali.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn