MRADI WA EACOP WAFIKIA ASILIMIA 81 KUKAMILIKA-MAKAME
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Bw. Mussa Makame amesema shirika hilo linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati katika sekta ya mafuta na gesi asilia ili kuimarisha usalama wa nishati nchini, kukuza uchumi na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania hususan vijana.
.
Akizungumza katika ukumbi wa Idara ya Habari – Maelezo uliopo Mtumba jijini Dodoma Machi 11, 2026, amesema moja ya miradi mikubwa inayoendelea ni wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki ambapo TPDC inamiliki asilimia 15 ya mradi huo.
.
Amesema mradi huo unaohusisha usafirishaji wa mafuta ghafi kutoka Hoima hadi Bandari ya Tanga umefikia asilimia 81 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Julai 2026.
.
Aidha, Serikali ipo katika hatua za mwisho za majadiliano ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa Mradi wa Gesi Asilia Kimiminika wenye thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 42, ambao unatarajiwa kuweka historia katika sekta ya nishati na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya gesi katika ukanda na kimataifa.
.
Ameeleza kuwa kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi asilia kutafungua fursa nyingi za ajira, zabuni za huduma na ushiriki wa wazawa kupitia sera ya Local Content.
.
Kwa upande mwingine, TPDC inaendelea na mradi wa uchongaji wa visima vitatu vya gesi katika eneo la Mnazi Bay ambao umefikia asilimia 27 ya utekelezaji.
.
Mradi huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa gesi kwa takribani futi za ujazo milioni 45 kwa siku.
.
Ukamilishaji wa mradi huo utachangia kuimarisha uzalishaji wa umeme pamoja na matumizi ya gesi katika viwanda na majumbani.
.
Vilevile, kuna mradi wa maendeleo ya gesi katika kitalu cha Ruvuma Basin katika eneo la Ntorya unaohusisha uchongaji wa visima vipya, ukarabati wa visima vilivyopo pamoja na ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi lenye urefu wa kilometa 34.2 kutoka Ntorya hadi Madimba.
.
Mradi huo wa bomba la gesi unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa gesi kwa takribani futi za ujazo milioni 60 kwa siku na kufungua fursa zaidi za maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa Ntorya na maeneo ya jirani.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

