OCPD YAWANOA WAANDISHI KUHUSU MAGEUZI YA SHERIA TANZANIA
Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) imeendesha mafunzo maalum kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uelewa wa kina kuhusu majukumu ya Ofisi, mwelekeo wake wa kimkakati pamoja na maandalizi ya kukabiliana na mabadiliko ya kisheria na kiteknolojia.
.
Mafunzo hayo yamelenga pia kuimarisha ushirikiano kati ya Ofisi na vyombo vya habari ili kuhakikisha taarifa za utekelezaji wa majukumu ya kisheria zinawafikia wananchi kwa usahihi na weledi.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Urekebu, Utafiti na Mafunzo, Bi. Rehema Katuga, amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alielekeza kutambuliwa kwa sheria zinazohitaji marekebisho ili ziendane na mahitaji ya sasa na mwelekeo wa Dira ya Maendeleo ya 2050.
Amesema tayari zoezi la kubaini sheria zilizopitwa na wakati limeanza, likilenga kuzifanyia urekebu ili ziweze kuendana na mazingira ya sasa.
.
Aidha, amesema kuwa OCPD ipo tayari kushirikiana na wizara na taasisi mbalimbali kutunga na kurekebisha sheria zitakazochochea utekelezaji wa Dira 2050.
Bi. Katuga ameongeza kuwa Ofisi imeanza kuandaa wataalamu katika masuala ya akili Unde (AI) na teknolojia, akibainisha kuwa ifikapo mwaka 2050 sehemu kubwa ya biashara itakuwa inaendeshwa kidijitali, hivyo maandalizi ya kisheria ni muhimu ili kukidhi mahitaji yatakayojitokeza.
Pia amesisitiza utayari wa OCPD kushughulikia mahitaji ya wizara na taasisi, hususan katika sekta binafsi, ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) pamoja na biashara, kwa lengo la kuimarisha mazingira ya uwekezaji na shughuli za kiuchumi.
Mafunzo hayo yameweka msingi wa uelewa mpana kuhusu nafasi ya Ofisi katika mageuzi ya sheria na maandalizi ya taifa kuelekea uchumi wa kidijitali, huku OCPD ikiahidi kuendelea kushirikiana na wadau ili kujenga mfumo wa kisheria thabiti, jumuishi na unaoendana na maendeleo ya nchi.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

