logo

WAZIRI MKENDA AMESEMA SERIKALI ITAENDELEA KUUNGA MKONO VYUO VINAVYOMILIKIWA NA TAASISI

SERIKALI imesema itaendelea kuunga mkono vyuo vikuu vinavyomilikiwa na taasisi za Dini na sekta binafsi kwa sababu vinachangia kutoa huduma ya elimu kwa watanzania.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda Mei 26, 2023 jijini Dodoma akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Philip Isdor Mpango katika uzinduzi wa jengo la utawala la Chuo Kikuu cha Mtakatifu John.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa katika kutekeleza hilo, Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan aliagiza zitengwe fedha katika Mradi wa HEET kwa ajili ya kufadhili masomo ya wahadhiri walioajiriwa kwenye vyuo vikuu binafsi ikiwa ni pamoja na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na taasisi za dini.

"Katika kutekeleza agizo la Rais wetu tumetenga jumla ya dola za kimarekani milioni moja kwa ajili ya kufadhilia masomo ya wahadhiri kutoka Vyuo Vikuu Binafsi katika Shahada za Uzamili na Uzamivu" amesisitiza Waziri Huyo.

Prof. Mkenda ameongeza kuwa mpaka sasa wahadhiri 27 wa vyuo vikuu binafsi wamenufaika na ufadhili huo, huku Chuo Kikuu cha Mtakatifu John nacho kikinufaika ambapo wahadhiri wake watatu wanasomeshwa katika ngazi Shahada za Uzamivu nje ya nchi.

Mkenda amekitaka Chuo Kikuu cha Mtakatifu John kuendelea kupanua zaidi uwezo wa kudahili kwa kuimarisha ubora wa mafunzo na kuongeza miundombinu ya chuo.

Aidha, amevitaka vyuo vikuu vyote nchini kuhakikisha vinasimamia ubora wa elimu inayotolewa ili kuzalisha wataalamu mahiri wenye weledi na kuwataka Wahadhiri kujikita katika kufanya utafiti.

@wizara_elimutanzania

#JordanMediaupdates

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn