SERIKALI YATANGAZA HATUA KUBORESHA USAFIRI WA WANAFUNZI MIJINI
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza hatua mbalimbali za kuboresha usafiri wa wanafunzi katika maeneo ya mijini, kufuatia malalamiko ya wanafunzi kunyimwa huduma na kunyanyaswa na wahudumu wa mabasi ya mijini (daladala).
Hatua hizo zimetangazwa leo Februari 04, 2026 jijini Dodoma, na Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame M. Mbarawa (Mb) wakati akizungumza na vyombo vya habari Dodoma, kufuatia kusambaa kwa video katika mitandao ya kijamii ya mwanafunzi Mariana Eric Mirindima, mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Jangwani, aliyelalamikia changamoto za usafiri wa wanafunzi.
Katika barua yake, mwanafunzi huyo ameeleza kuwa makondakta wa daladala wamekuwa wakigoma kuwabeba wanafunzi wakidai kuwa hawalipi nauli kamili, hali inayosababisha wanafunzi kusimama vituoni kwa muda mrefu, kuchelewa kufika shuleni au kushindwa kabisa kuhudhuria masomo.
.
Amesema hali hiyo inaathiri masomo yao, usalama wao na ustawi wao kwa ujumla.
.
Prof. Mbarawa amesema Serikali imesikiliza kilio cha wanafunzi na itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya watoa huduma wa usafiri wa umma wanaokiuka sheria na kanuni.
"Serikali, kupitia Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imeweka mikakati ya kuboresha usafiri wa wanafunzi ikiwemo kuanzisha mabasi maalumu ya wanafunzi nyakati za asubuhi na jioni, kutenga mabehewa maalumu ya wanafunzi katika treni za mijini Dar es Salaam, pamoja na kusimamia utozaji wa nauli maalumu ya Shilingi 200 kwa wanafunzi katika daladala na mabasi yaendayo haraka" alisema Prof. Mbarawa.
Aidha, Prof. Mbarawa ameiagiza LATRA kuharakisha zoezi la kuthibitisha madereva na kusajili makondakta nchini kote, kuimarisha udhibiti wa nauli na staha ya huduma kwa wanafunzi, pamoja na kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye vituo vya daladala, hususan nyakati za asubuhi na jioni.
Serikali pia imewataka wananchi kushirikiana kwa kutoa taarifa za ukiukwaji wa haki za wanafunzi kupitia namba za bure na mitandao ya mawasiliano ya LATRA, ili kuhakikisha wanafunzi wanapata usafiri salama, wa haki na unaowawezesha kupata elimu bila vikwazo.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

