logo

SERIKALI YAPONGEZA MCHANGO WA LALJI FOUNDATION KWENYE SEKTA YA ELIMU

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za Taasisi ya Lalji Foundation katika kuimarisha elimu na maendeleo ya kijamii, hususan kuhakikisha watoto wanapata elimu bora, jumuishi na yenye usawa.

‎Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo Januari 10, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya ugawaji wa vifaa vya shule kwa wanafunzi kutoka vituo vya kulea watoto yatima, akibainisha kuwa Serikali inautambua na kuuthamini mchango mkubwa wa taasisi hiyo katika ujenzi wa shule pamoja na utoaji wa misaada inayochochea maendeleo ya elimu nchini.

‎Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza sera ya elimu bila ada kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita, sambamba na kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wenye uhitaji ili kuhakikisha hakuna mtoto anayenyimwa fursa ya kupata elimu.

‎Kwa upande wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakar Zuber Ali Mbwana, ameipongeza Taasisi ya Lalji Foundation kwa jitihada zake za kuwasaidia watoto yatima na wasiojiweza, akisisitiza kuwa matendo hayo ni ya kiutu, ya mfano na yenye thawabu kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

‎Naye Mlezi wa Taasisi hiyo, Ndg. Mohsin Lalji, amesema Taasisi imewapatia wanafunzi 400 wa shule za msingi vifaa vya shule ikiwemo sare, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuboresha mazingira ya kujifunzia.

‎Ameongeza kuwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika sekta ya elimu, Taasisi ya Lalji Foundation pia imechangia madawati 300 kwa shule mbalimbali zenye uhitaji.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn