MAZINGIRA SALAMA NA SHIRIKISHI YASIYO NA UKATILI WA KIJINSIA NI NJIA SAHIHI YA KUONDOA UKATILI NCHINI-WAKILI MPANJU
Imeelezwa kuwa mazingira salama na shirikishi yasiyo na ukatili wa kijinsia hususani kwa wanawake na wasichani ni njia sahihi ya kuondoa ukatili wa kijinsia nchini Tanzania.
kutokana na hilo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeandaa kikao cha tatu cha Kamati Tendaji ya Mpango wa Taifa wa Usawa wa Kijinsia kwa lengo la kuonesha mafanikio,changamoto na hatua zinazochukuliwa katika kuendeleza usawa wa kijinsia hapa nchini.
Aidha,Kikao hicho, ambacho ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Mageuzi ya Usawa wa Kijinsia (Gender Transformative Action Programme 2021–2027) unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), kimefanyika leo Mei 29,2025 jijini Dodoma ambapo kimehudhiriwa na washiriki zaidi ya 65 kutoka serikalini, sekta binafsi, taasisi za kiraia, na wafadhili wa maendeleo.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju amefurshishwa kuwa sehemu ya kikao hicho ambapo amesema kikao hicho kimetoa fursa ya kubuni njia za mabadiliko katika utoaji wa huduma za kijinsia, kujenga imani kwa wahanga, na kuimarisha mbinu za kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia nchini.
Kwa upande wake, Karina Dzialowska, Mkuu wa Idara ya Uchumi na Utawala Bora katika Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania amesema wametimiza miaka miwili ya utekelezaji, na kikao hicho kimewapa nafasi ya kuonyesha mafanikio, changamoto na mipango ya baadaye.
Naye Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Lucy Uisso, amesema mafanikio katika uelewa wa haki za wanawake yanaonekana kupitia kesi zinazofikishwa mahakamani.
"Kwa sasa idadi ya wanaofikishwa mahakamani kwa makosa ya ukatili imeongezeka, huku wengi wao wakitiwa hatiani. Hii ni dalili njema kuwa haki inatendeka.". Amesema
Kadhalika,Msaada huo unatekelezwa kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wizara ya Afya, Wizara ya Katiba na Sheria (kupitia Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Mahakama), na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Zanzibar pia imenufaika kupitia bajeti maalum ya Euro milioni 7 inayoendeshwa kwa ushirikiano na UN Women.
Mpango huu unachangia moja kwa moja katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III 2021/22–2025/26) na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, ambazo zimeweka usawa wa kijinsia kama kipaumbele kikuu katika maendeleo ya taifa.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

