RAIS MUSEVENI AWAZAWADIA WABUNGE WA UGANDA SHILINGI MILIONI 100 KILA MMOJA
Rais wa Uganda Bw. Yoweri Museveni ameripotiwa kuwazawadia Wabunge wa Uganda takribani shillingi milioni 100 za Uganda ( sawa na shilingi milioni 64 za Kitanzania) kila mmoja kama ishara ya kushukuru kile wadadisi wa mambo walichokitaja kuwa "tabia njema."
Kulingana na gazeti la Daily Monitor, pesa hizo ziligawiwa kimyakimya Jumapili, Aprili 6, 2025, katika kile ambacho kimezua ghadhabu na mijadala ya umma kuhusu uadilifu wa uongozi wa bunge la Uganda.
Wabunge wengi, kutoka chama tawala, huru na upinzani, wamethibitisha kupokea fedha hizo kutoka kwenye Ofisi ya Mnadhimu Mkuu wa Serikali Bungeni au moja kwa moja kutoka kwa Spika Anita Among katika makazi rasmi ya Nakasero.
Ulipaji unaodaiwa unasemekana ulifanyika kati ya saa 2 asubuhi hadi saa 3 asubuhi siku ya Jumapili, kwa njia iliyoratibiwa na ya busara.
Wakosoaji wamesema kuwa utoaji wa fedha nyingi kwa wabunge hasa katika uchumi ambapo wananchi wa kawaida wanatatizika na mfumuko wa bei, kodi kubwa na masuala ya utoaji huduma ni sawa na matumizi mabaya ya wazi ya fedha za umma.
Ingawa baadhi ya wabunge walitetea kitendo hicho, wakisema ni pesa za kibinafsi za Rais Museveni na zililenga kuwasaidia katika nyakati ngumu za kiuchumi, wengine walikiri kwa faragha kutoridhika na kutiliwa shaka kuhusiana na mchakato huo.
Kufikia Jumatano, hakuna maelezo rasmi au taarifa yoyote ilikuwa imetolewa na Ikulu ya Uganda au ofisi ya Spika kufafanua chanzo na madhumuni yaliyokusudiwa ya fedha hizo.
Raia wengi wa Uganda wamejitokeza kwenye mitandao ya kijamii kueleza hasira na kutoamini juu ya ufichuzi huo, wakitaka uwajibikaji na uchunguzi kuhusu suala hilo.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

