TUNATAKA MAENDELEO KWA AJILI YA WATU WETU - DKT. BITEKO
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)Taifa ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2024, CCM imedhamiria kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ili kubadilisha hali za maisha ya wananchi.
Amesema Kata ya Namonge ni kati ya kata 17 za Wilaya ya Bukombe yenye vijiji vinane na vitongoji 36 ambayo imeendelea kupiga hatua ya maendeleo kwa kuwa na mtandao mrefu zaidi wa barabara kuliko kata zingine.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Novemba 25, 2024 wakati akihutubia katika Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wilayani Bukombe zilizofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Namonge mkoani Geita.
“ Tunataka maendeleo kwa ajili ya watu wetu na kata hii imeandikisha idadi kubwa ya wananchi leo nimekuja kuwaomba mchague viongozi wa CCM ili tuendeleze jitihada zetu za kuwaletea maendeleo,” amesema Dkt. Biteko.
Ametaja miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika kata hiyo kuwa ni ujenzi wa shule za tatu za sekondari, zahanati nne na kituo cha afya kimoja.
“ Awali tulikuwa na barabara kutoka Uyovu hadi Namonge na barabara ya kwenda maeneo mengine haikuwa nzuri, barabara ya kutoka Namonge hadi Mjimwema haikuwepo. Hatua iliyopigwa ni kubwa na leo tumekuja na kazi moja ya kuomba kura zenu wananchi wa Namonge,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Amebainisha mipango ya maendeleo ya baadae kuwa ni kujenga shule ya sekondari na kuimarisha hospitali ili iweze kutoa huduma za upasuaji katika kata hiyo.
Ameendelea kusema ili kufanya kazi vizuri zaidi ni vyema kupata viongozi wa vijiji na vitongoji wanaotokana na chama kimoja kwa vile wanauhusiano mzuri wa kazi na hivyo kurahisisha juhudi za kuleta maendeleo kwa wananchi.
Pamoja na hayo, Dkt. Biteko amewahimiza wananchi wa Bukombe na Watanzania wote kwa ujumla kujitokeza kwa wingi na kupiga kura ili kuchagua viongozi wao.
“ Tunatambua uchaguzi huu ni muhimu na sisi tunausimamia kwa haki ili kupata viongozi watakaotatua shida za wananchi,” amebainisha Dkt. Biteko.
Naye, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Bukombe, Matondo Lutonja amesema itakapofika siku ya kupiga kura Novemba 27, 2024 wananchi wa Bukombe wajitokeze kwa wingi ili kutimiza haki yao ya kikatiba.
Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini zitahitimishwa Novemba 26, 2024 na mkoani Geita kampeni hizo zitafanyika Kata ya Runzewe Magharibi ambapo Dkt. Biteko atakuwa mgeni rasmi.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news