logo

SELF MF, WODESU WACHOCHEA UJASIRIAMALI WA WANAWAKE DODOMA ‎

WANAWAKE wajasiriamali 1,450 jijini Dodoma wamepata fursa ya kukuza biashara zao kupitia mikopo ya Self Microfinance Fund (SELF MF) inayotolewa kwa kushirikiana na Wodesu Microcredit, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya mitaji inayowakabili wafanyabiashara wadogo, wakiwemo wauzaji wa mboga za majani.

‎

‎Akizungumza katika ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya SELF MF jijini Dodoma Mkurugenzi Mtendaji wa Wodesu Microcredit, Melina Faustine, amesema mikopo hiyo imeongeza uwezo wa taasisi yake kuwafikia wanawake wengi zaidi ambao wamekuwa na changamoto ya kupata huduma za kifedha kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

‎

‎Amesema ushirikiano huo umekuwa muhimu katika kupanua wigo wa utoaji wa mikopo kwa wanawake wajasiriamali, hususan wale wanaofanya biashara ndogo ndogo.

‎

‎“Kupitia mikopo ya SELF MF imenisaidia kufikia wanawake wengi zaidi. Mpaka sasa nimeweza kuwafikia wanawake 1,450, wakiwemo wale wanaouza mboga za majani ambao si rahisi kupata mikopo katika sehemu nyingine,” amesema.

‎

‎Hata hivyo, Faustine amesema baadhi ya waombaji wamekuwa wakiwasilisha biashara ambazo si zao wanapoomba mikopo, hali inayoweza kuathiri matumizi ya fedha na kusababisha changamoto katika urejeshaji.

‎

‎Ameeleza kuwa ni muhimu waombaji kuwa waaminifu katika taarifa wanazowasilisha ili mikopo itolewe kwa walengwa sahihi na kurejeshwa kwa wakati, hivyo kuwezesha fedha hizo kuendelea kuwanufaisha wajasiriamali wengine.

‎

‎Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya SELF MF, Paul Sangawa, amesema ziara hiyo imelenga kujionea namna mfuko huo unavyoshirikiana na taasisi za kifedha kufikisha huduma za mikopo kwa wananchi na kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

‎

‎Amesema taasisi kama Wodesu Microcredit zina nafasi muhimu katika kuwafikia wafanyabiashara wadogo, hasa wanawake wanaohitaji mitaji ya kuanzisha, kuimarisha na kupanua biashara zao.

‎

‎Sangawa amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mifumo madhubuti ya kufuatilia matumizi ya mikopo na marejesho yake ili fedha zinazorejeshwa ziweze kutumika tena kuwafikia wananchi wengine wenye mahitaji ya mitaji.

‎

‎“Wananchi wengi wana mahitaji ya mikopo na hii ni mojawapo ya fursa wanazoweza kuzitumia kujikwamua kiuchumi na kuanzisha shughuli mbalimbali zinazoweza kuwasaidia kuboresha maisha yao,” amesema.

‎

‎Naye Msemaji Mkuu wa SELF MF, Santieli Yona, amesema mfuko huo una mikopo ya aina mbalimbali inayolenga kukidhi mahitaji ya makundi tofauti ya wananchi, yakiwemo wakulima, wafanyabiashara, wafanyakazi wa Serikali na taasisi za kifedha.

‎

‎Amesema mfuko huo hutoa mikopo kwa taasisi za kifedha zilizosajiliwa kisheria, vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS), pamoja na mikopo ya moja kwa moja kwa watu binafsi kulingana na aina ya huduma na vigezo vinavyotumika.

‎

‎Yona amewahimiza Watanzania kutumia fursa za mikopo zinazotolewa na SELF MF kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa na kuandaa mipango madhubuti ya biashara itakayowawezesha kutumia mitaji kwa tija.

‎

‎“Tunakaribisha Watanzania wote waje SELF MF kwa sababu tuna mikopo ya aina mbalimbali kwa ajili ya biashara na shughuli tofauti za kiuchumi. Lengo letu ni kuwawezesha wananchi kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao,” amesema.

‎

‎Amesisitiza kuwa uelewa wa masharti ya mikopo na usimamizi mzuri wa fedha ni mambo muhimu katika kuhakikisha mitaji inayopatikana inachangia ukuaji wa biashara, ongezeko la kipato na urejeshaji wa mikopo kwa wakati.

‎

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn