TANZANIA YAWASILISHA TEKNOLOJIA YA KUKADIRIA ATHARI ZA MAGARI YA UMEME
Tanzania imeendelea kutoa mchango katika kuimarisha mifumo endelevu ya ufadhili wa matengenezo ya barabara barani Afrika kupitia uwasilishaji wa uzoefu wa matumizi ya programu ya Electric Vehicle (EV) Impact Simulator katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 23 wa ARMFA jijini Nairobi, Kenya.
.
Katika kikao hicho, Mhandisi Dkt. Joshua Mwankunda wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Tanzania aliwasilisha uzoefu wa matumizi ya programu hiyo, akieleza namna inavyotumia takwimu kukadiria upungufu wa mapato ya matengenezo ya barabara unaoweza kusababishwa na ongezeko la magari ya umeme, pamoja na kufanya majaribio ya sera na mbinu mbadala za kukabiliana na upungufu huo.
.
Programu hiyo iliyotengenezwa kwa msaada wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi kwa Afrika (UNECA), ilikabidhiwa rasmi kwa ARMFA na kupokelewa kwa niaba ya nchi wanachama na Rais wa ARMFA, Mhandisi Rashid Selemani Kalimbaga, ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Tanzania.
.
Teknolojia hii ni hatua muhimu katika kuziandaa nchi za Afrika kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia ya usafiri na kuhakikisha mifumo ya upatikanaji wa fedha za matengenezo ya barabara inabaki kuwa endelevu, bila kujali aina ya nishati inayotumika katika vyombo vya usafiri.
.
Tanzania inaendelea kushiriki katika kuandaa suluhisho za kesho kwa ajili ya barabara za Afrika.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

