DMF YAFANIKIWA KUZIFIKIA HOSPITALI 85 NCHINI NA KUCHANGIA VIFAA VYENYE GHARAMA YA SH.BILIONI 1.5
Kila ifikapo Novemba 17 kila mwaka, dunia huadhimisha siku ya Mtoto NJITI duniani, ambapo siku hii ilianzishwa kwa nia ya kuelimisha jamii kuhusu kujifungua watoto njiti ambao hawajakomaa na kufikisha wiki 37.
.
Katika kuadhimisha siku hii, Daktari Bingwa wa watoto nchini Dkt. Albert Chotta amesema kwamba, kila sehemu ambapo wakinamama wajawazito wanajifungua lazima kuwepo na huduma za msingi (hususani za mtoto njiti) na kama zisipokuwepo hiyo sio huduma, hivyo amewataka waandishi wa habari kutilia mkazo katika eneo hilo kupitia kalamu zao.
.
Dkt.Chotta ameyasema hayo Novemba 16,2024 Jijini Dar Es Salaam alipokuwa kwenye Semina Maalum ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari katika kuripoti taarifa kuhusu watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (NJITI) iliyoandaliwa na Taasisi ya Doris Mollel (DMF) iliyofanyika katika Ukumbi wa Sheraton Hotel.
.
Amesema Serikali imejiwekeza katika kuwajengea uwezo watoa huduma ili kuweza kupata ujuzi na uwezo wa kutoa huduma za watoto wachanga nchini.
.
"Sio wahudumu wote ambao wanaweza kuwasaidia watoto njiti, hawa watoto ni maalum wanahitaji uangalizi maalum, kwahiyo tunawafundisha wahudumu ili waweze kutoa huduma za watoto njiti" alisema Dkt.Chotta.
.
Amesema wazazi wenye watoto njiti wanapaswa kuwasaidia viongozi wa serikali kwa kupaza sauti zao ili waweze kupewa kipaumbele watoto hao katika utoaji wa huduma.
.
"Tatizo la watoto njiti nchini ni kubwa, lilikuwepo, lipo na litaendelea kuwepo. Takwimu zinasema katika kila watoto 10 wanaozaliwa hospitalini, lazima atakuwepo mtoto mmoja njiti" alisema.
.
Aidha, Dkt.Chotta ameiomba serikali kufanya uchechemuzi ili zile huduma stahiki na mazingira wezeshi yapelekwe katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma za kuwasaidia akinamama wanaojifungua watoto njiti.
.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo ya DMF, Dkt.Sylvia Ruambo, amesema kupitia taasisi ya Doris Mollel, mpaka hivi wamefanikiwa kuzifikia hospitali takribani 85 nchini, na wamechangia vifaa vyenye gharama ya shiling Bilioni 1.5.
.
"Jamii inapaswa kutambua kwamba, mtoto njiti anapozaliwa tu mama asinyanyapaliwe,asihusishwe na masuala ya imani za kishirikina, kwani mtoto njiti sio kosa la mama,ni mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati wake hiyo ndio tasfiri sahihi" alisema Dkt.Sylvia.
.
Kwa upande mwingine, Dkt.Sylvia amesema wamefanikiwa kuingiza elimu ya mtoto njiti katika mtaala wa sayansi shuleni ambapo walikaa pamoja na taasisi ya elimu Tanzania (TIE) na kuangalia namna ambavyo mtaala wa Watoto njiti unaweza ukaingizwa katika masomo ya sayansi.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news