logo

BMH IMEFANIKIWA KUFANYA UPASUAJI WA MOYO KWA WATU ZAIDI YA 40 - PROF.MAKUBI

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa(BMH) Prof. Abel Makubi amesema tatizo la ugonjwa wa moyo hapa nchini Tanzania linawaathiri sana kundi la vijana hususani wenye umri kuanzia miaka 30 hadi 40 huku mataifa ya ulaya wao wakianzia miaka 50 hadi 60.

Prof.Makubi ameyasema hayo leo Oktoba 01,2024 jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali hiyo baada ya madaktari bingwa kutoka nchini Uholanzi kuweka kambi BMH kwa muda wa wiki tatu kuanzia leo mpaka tarehe 21 Oktoba, 2024 kwa ajili ya matibabu ya moyo kwa watu wazima ikijumuisha uchunguzi, uzibuaji wa mishipa ya moyo na upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua.

Amesema kuwa, tatizo hilo linatokana na baadhi ya watu kushindwa kubadili tabia ya mtindo wa maisha, hivyo ameitaka jamii kufuatilia elimu inayotolewa na wataalamu mara kwa mara ili waweze kujikinga na tatizo la Moyo.

.

"Serikali inafanya jitihada kupitia kitengo chake cha NCD kufanya kampeni nyingi sana za kuelimisha watu wabadilishe tabia za ulaji, mazoezi,uvutaji wa sigara,pombe,chumvi na mafuta. Hivyo wananchi wawe wasikivu kwenye elimu inayotolewa ili tusipate magonjwa haya ya Moyo, na yanayosababisha tatizo la moyo kama kisukari na Presha" alisema Prof.Makubi.

.

Kwa upande mwingine, Prof.Makubi amesema mpaka hivi sasa hospitali hiyo imefanikiwa kufanya upasuaji wa moyo kwa watu zaidi ya 40 kwa watoto na watu wazima, na BMH ilifungua Idara ya Moyo mwaka 2019 na ilipofika 2021 ikawa na kitengo cha Upasuaji wa moyo na kifua na mpaka hivi sasa wamekuwa wakitoa huduma hiyo katika kuchunguza, kutibu na kupasua watu wenye matatizo ya Moyo

.

Aidha,Prof.Makubi amesema madaktari hao pia wametoa vifaa vya shiling milioni 400 ili kusaidia kupunguza gharama ya matibabu kutokana na huduma ya moyo kuwa ghali hapa nchini.

.

Naye Mkuu wa Idara Kitengo cha upasuaji Moyo Dkt.John Meda amesema Bima ya Afya ya NHIF imekuwa mkombozi kwa wagonjwa wengi hapa nchini, hivyo ametoa wito kwa wananchi kujiunga na Bima hiyo kwa Sababu itapunguza gharama za matibabu ya magonjwa sugu.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn