
DKT.BITEKO AZINDUA UJENZI MRADI WA UMEME MALAGARASI 49.5 MW KIGOMA
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha linatekeleza kwa kasi miradi ya umeme itakayounganisha Mkoa wa Kigoma katika gridi ya Taifa ifikapo mwishoni mwaka huu Mkoa huo usitumie umeme unaozalishwa kwa kutumia mafuta mazito.
Ametoa agizo hilo tarehe 19 Septemba 2024 mkoani Kigoma wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi mradi wa uzalishaji umeme katika mto Malagarasi (49.5 MW), uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kV132 kutoka Igamba hadi Kidahwe na Kituo cha kusambaza umeme msongo wa kV 400/220/132/33 cha Kidahwe.
Amesema kuwa, Serikali imekuwa ikitumia shilingi bilioni 35 kwa mwaka kwa ajili ya kununua mafuta kwa kuendeseha majenereta ya kuzalisha umeme huku makusanyo yakiwa ni shilingi bilioni 16 hivyo imekuwa ni hasara kwa Shirika.
Amesema zoezi hilo la uzimaji wa majenereta pia litafanyika kwa mikoa ambayo haijafikiwa na umeme wa gridi.
Ameeleza kuwa, Kigoma inaingia kwenye historia ya kuwa na umeme wa gridi wa uhakika kwa kuwa itapata umeme kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo kutoka Nyakanazi kwa msongo wa kV 400 na kV 220, njia nyingine ni kutoka chanzo cha Malagarasi hadi Kidahwe, kutokea Katavi kwa msongo wa kV 400 na laini ya SGR kutoka Dar es Salaam ya kV 220.
Dkt. Biteko amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Kigoma ambapo katika Sekta ya Nishati ametoa zaidi ya shilingi trilioni 1.2 katika mwaka wa fedha 2024/2025 ili kutekeleza miradi ya umeme.
Ameeleza kuwa, kwa umeme wa gridi kufika Kigoma Mkoa huo sasa unaondoka kwenye historia ya kuitwa mkoa wa pembezoni na kutambulika kama Mkoa wa maendeleo.
Kuhusu kazi ya usambazaji umeme vijijini amesema Vijiji vyote vitapata umeme kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Katika hatua nyingine Dkt.Biteko ametoa mifuko 500 ya simenti ili kuunga mkono juhudi za wananchi ambao wameanza kujenga kituo cha afya katika Kata ya Kidahwe huku akiahidi kuwa Serikali itajenga kituo kingine cha afya.
Aidha katika Kijiji cha Igamba ambapo kunatekelezwa mradi wa Malagarasi amesema itajengwa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Barabara ya lami ya kilometa 20 .
Dkt. Biteko pia ameipongeza TANESCO kwa kubadilika katika utrendaji kazi kwa kujikita katika kupelekea watu umeme ambapo amewataka wasirudi nyuma na kwamba anaona fahari kuongoza Shrika hilo kwa sasa.
Aidha, kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa amewaasa wananchi kuchagua viongozi kutokana na uwezo wao wa kuwahudumia na siyo kigezo cha fedha.
Tranding News

Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news