logo

DKT.BITEKO AIPONGEZA REA KWA KUPELEKA NA KUSAMBAZA NISHATI VIJIJINI

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Mashaka Biteko jana, tarehe 20 Agosti, 2024 ameshuhudia tukio kubwa la kihistoria baada ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kusaini mikataba ya kupeleka nishati ya umeme kwenye vitongoji 3,060 vya Tanzania Bara, tukio liliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma.

“Kipekee ninaipongeza Bodi ya Nishati Vijijini (REB) pamoja na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa juhudi kubwa ya kuhamasisha, uwekezaji na uwezeshaji wa upatikanaji wa umeme kwenye maeneo ya vijijini, sisi sote ni mashahidi kuwa vijiji vyetu vimekuwa na kasi ya maendeleo kutokana na uwepo wa umeme unapolekwa kupitia Miradi inayotekelezwa na REA”.

“Tunafahamu kuwa Wakala (REA) upo katika hatua ya mwisho ya kukamilisha safari ya kupelekea umeme vijijini, na kama tulivyofahamishwa, vijiji vilivyosalia, ambavyo havijafikiwa na umeme ni 151 ambapo inatarajiwa hadi tarehe 30 Septemba, 2024 viwe vimekamilika, kwa sasa Serikali inahama kutoka kwenye kupeleka umeme kwenye vijiji hadi kwenye vitongoji, jambo ambalo safari yake ndiyo imeanza leo.” Amekaririwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko.

Dkt. Biteko ameongeza kuwa, Mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji utatekelezwa kwa awamu ambapo, leo inashuhudiwa vitongoji takribani 3,060 vitapatiwa umeme kupitia mradi huu kwa gharama ya Jumla ya bilioni 362.

“Kwa takribani miaka 17 hadi sasa, Serikali imekuwa ikishirikiana na Wabia wa Maendeleo katika utekelezaji miradi mbalimbali ya kimkakati ya nishati vijijini.” Amesema Dkt. Biteko.

"Mikataba hii tuliyoishudia leo yenye jumla ya shilingi bilioni 362.8 imewezeshwa kupitia ushirikiano baina ya Serikali na Benki ya Dunia. Hivyo, kwa niaba ya Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, naomba niwashukuru Washirika wa Maendeleo wanaochangia katika mfuko wetu wa Nishati Vijijini, hususan Benki ya Dunia, Serikali za Norway na Sweden, Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), Shirika la Fedha Duniani (IMF), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD)," amesema Dkt. Biteko.

"Wananchi wanatarajia kunufaika na mradi huu wanayo matarajio makubwa kuwa upatikanaji wa nishati ya umeme utaboresha na kuinua hali zao za maisha kupitia ushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Niwahakikishie Wananchi wote kuwa Serikali itaendelea kutenga fedha, na kushirikiana na wabia wa maendeleo kuhakikisha kuwa umeme unawafikia Watanzania wote, popote walipo, " ameongeza Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Dkt. David Mathayo David ameipongeza Serikali kwa juhudi za makusudi za kusambaza umeme kwenye vitongoji 3,060 jambo ambalo linakwenda kutekelezwa sasa na REA.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy, amesema hadi kufikia Desemba 2024, vijiji vyote vya Tanzania Bara 12,318 vitakuwa vimefikiwa na huduma ya umeme, hatua ambayo itaongeza hali ya upatikanaji wa umeme katika maeneo ya vijijini.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn