WAKANDARASI TUMIENI VYEMA FURSA ZA BENKI -KASEKENYA
Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amewataka Wakandarasi nchini kutumia vizuri fursa za benki kukuza mitaji na hivyo kumudu kupata miradi mikubwa ya ujenzi ili kukuza uchumi binafsi na taifa kwa ujumla.
Akizindua mkakati wa masuluhisho bora kwa Wakandarasi yanayotolewa na benki ya NMB jijini Dar es salaam leo Naibu Waziri Kasekenya amesema fursa hizo zinaendana na mikakati ya Serikali ya kukuza uchumi wa Wakandarasi wazawa ili fedha nyingi za miradi ya ujenzi zibaki nchini.
" Uaminifu, weledi na uzalendo kwa Wakandarasi kutawezesha benki nyingi kutoa mikopo na fursa nyingi na kukuza sekta ya Wakandarasi", amesisitiza Eng. Kasekenya.
Ameipongeza benki ya NMB kwa mikakati yake ya kuwawezesha Wakandarasi hususan wazawa hali itakayokuza sekta ya ujenzi nchini.
" Serikali inatarajia fursa hizi na nyingine zitakazotolewa zitawawezesha Wakandarasi wazawa kushindana na Wakandarasi wa nje na kupata miradi mikubwa ya ujenzi na hivyo kuongeza ujuzi katika ujenzi wa miradi na kutoa fursa nyingi za ajira", amesisitiza Naibu Waziri huyo.
Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bw, Filbert Mponzi amesema NMB imejipanga kuhakikisha inakuza wakandarasi hususan wakandarasi wadogo ili kukuza sekta ya ukandarasi na ujenzi kwa ujumla.
Masuluhisho yatakayowanufaisha wakandarasi ni pamoja dhamana za Benki, mikopo ya haraka na hati za kifedha za dhamana zitakazowezesha wakandarasi waliopata miradi kupata fedha za ujenzi kwa haraka na nafuu.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

