logo

PPRA,NMB WAZINDUA HUDUMA YA UHAKIKI WA DHAMANA ZA ZABUNI

Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa kushirikiana na NMB Bank Plc wamezindua rasmi huduma ya kidijitali ya uhakiki wa dhamana za zabuni za kibenki kupitia Mfumo wa NeST (National e-Procurement System of Tanzania), hatua inayotarajiwa kuongeza uwazi, kasi na usalama katika mchakato wa zabuni za umma nchini.

‎.

‎Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika Machi 05, 2026 katika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba, amesema kuunganishwa kwa Mfumo wa NeST na mifumo ya benki ni mapinduzi makubwa katika usimamizi wa ununuzi wa umma, yaliyowezeshwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

‎.

‎Amesema huduma hiyo itawezesha dhamana za zabuni zinazotolewa na NMB kuthibitishwa moja kwa moja kupitia mfumo wa NeST, bila taasisi nunuzi kuhitaji kuwasiliana na benki kwa njia ya barua kama ilivyokuwa hapo awali.

‎.

‎“Mzabuni ataingiza namba ya dhamana aliyopata kutoka benki kwenye mfumo wa NeST, na mfumo utaivuta dhamana hiyo moja kwa moja kutoka benki husika na kuiwasilisha kwa taasisi nunuzi. Hatua hii imeondoa mianya ya kughushi na kuongeza ufanisi katika mchakato wa zabuni,” alisema Simba.

‎.

‎Ameongeza kuwa hatua hiyo inaendana na maono ya serikali ya kujenga uchumi wa kidijitali na kuboresha mazingira ya biashara nchini.

‎.

‎Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, amesema kupitia mfumo huo PPRA na NMB watahakiki dhamana za zabuni pamoja na akaunti ya mzabuni na kutoa majibu papo hapo.

‎.

‎“Leo tunazindua rasmi suluhisho la ‘Digital Bank Guarantee Confirmation’ kwa kushirikiana na PPRA. Mfumo huu utarahisisha na kuharakisha michakato ya ununuzi wa umma kuanzia usajili, zabuni, mikataba hadi malipo kupitia mfumo wa NeST,” alisema Zaipuna.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn