logo

ALIYEMTUKANA RAIS MUSEVENI TIKTOK,AHUKUMIWA MIAKA 6 JELA

Mahakama nchini Uganda imemhukumu mtayarishaji wa maudhui mtandaoni Edward Awebwa, mwenye umri wa miaka 24, kifungo cha miaka sita jela kwa kumtukana Rais Yoweri Museveni na familia yake kupitia video iliyowekwa kwenye akaunti yake ya TikTok.

Bw. Awebwa ameshtakiwa kwa matamshi ya chuki na kueneza taarifa za kupotosha na zenye nia mbaya dhidi ya Rais Yoweri Museveni, Mke wa Rais Janet Museveni, na mtoto wao Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mkuu wa Jeshi.

Zaidi ya hayo, mtayarishaji wa maudhui huyo pia ameshutumiwa kwa kuchapisha taarifa za matusi, akisema kwamba kumekuwa na ongezeko la kodi chini ya Rais Museveni.

Hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo Bi.Stella Maris Amabilis alisema kuwa wakati Awebwa aliomba kusamehewa, alishindwa kuonyesha majuto kwa kitendo chake, na maneno yaliyotumika kwenye video hiyo ni machafu sana.

"Mshtakiwa anastahili adhabu ambayo itamwezesha kujifunza kutokana na maisha yake ya nyuma ili wakati ujao aheshimu utu wa rais, mke wa rais na mtoto wa kwanza wa kiume," alisema Hakimu Stella Maris Amabilis.

Amehukumiwa kifungo cha miaka sita kwa kila moja ya mashtaka manne yanayomkabili, ambayo yataendeshwa kwa wakati mmoja.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn