logo

WATUHUMIWA 12 WA DAWA ZA KULEVYA WAFIKISHWA MAHAKAMANI

𝐖𝐚𝐭𝐮𝐡𝐮𝐦𝐢𝐰𝐚 𝟏𝟐 𝐰𝐚 dawa za kulevya jana tarehe 22 Aprili, 2024 wamefikishwa katika Mahakama za Hakimu Mkazi Kibaha Mkoani Pwani na Kisutu jijini Dar es salaam wakikabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya.

Wakisomewa mashtaka yao katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Joyce Mkhoi na Wakili wa Serikali, Agness Ndanzi, alidai mahakamani hapo kuwa, washtakiwa Rajabu Kisambwanda (42) mkazi wa Kerege Matumbi, Bakari Said (39) Mkazi wa Kunduchi Mtongani na Hillary Rhite (35) Mkazi wa Kunduchi Sodike walikamatwa eneo la Zinga Bagamoyo wakiwa na dawa za kulevya aina ya Methemphetamine Kilo 424.84 pamoja na Heroin Hydrochloride gramu 158.24.

Aidha,siku hiyohiyo mshtakiwa Bakari Said (39) Mkazi wa Kunduchi Mtongani alikutwa akisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin hydrochloride yenye uzito wa gramu 158.24.

Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, watuhumiwa tisa (9) wamefikishwa Mahakamani hapo jana tarehe 22 Aprili, 2024 wakikabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin na methamphetamine zenye uzito wa kilogramu 332.

Akisoma mashtaka yao mbele ya mahakama hiyo, wakili wa serikali Batilda Mushi amewataja washtakiwa hao kuwa ni Ally Ally @kabaisa (28), Bilali Hafidhi (31), Mohamed Hamisi (47), Idrisa Mbona (33), Rashid Rashid (24), Shabenga Shabenga (24), Dunia Mkambilah (52), Mussa Hussein (35) na Hamis Omary (25).

Amesema katika shtaka la kwanza, washtakiwa walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Methamphetamine kiasi cha kilgramu 100.83 karibu na hotel ya white sands wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Katika shtaka la pili katika eneo hilohilo, washtakiwa walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin hydrochloride kiasi cha kilogramu 232.69.

Hata hivyo, washtakiwa wote hawakuruhusiwa kujibu chochote kwani Mahakama hizo hazina mamlaka kisheria kusikiliza mashauri hayo.

Washtakiwa wote wamerudishwa mahabusu kutokana na kesi zinazowakabili kutokuwa na dhamana hadi tarehe 6 na 7 Mei,2024 kwa kutajwa.

#JordanMediaupdates

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn