MRADI WA KITUO CHA SARATANI BENJAMIN MKAPA HOSPITAL WAFIKIA ASILIMIA 61-DKT.HUMBA
Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) Kanda ya Afrika, Bw. Gashaw Wolde, ameipongeza Serikali ya Tanzania pamoja na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa katika sekta ya afya, hususan kuimarisha huduma za matibabu ya saratani.
.
Bw. Wolde ameyasema hayo leo Februari 03,2026 alipokuwa ametembelea ujenzi wa mradi wa kituo cha Umahiri cha Mafunzo na Matibabu ya Saratani kinachojengwa katika Hospitali hiyo.
.
Bw. Wolde amesema kukamilika kwa kituo hicho kutaifanya Tanzania kuwa kitovu kikubwa cha huduma za matibabu kwa nchi jirani, hatua itakayochochea pia ukuaji wa tiba utalii.
.
"Uwekezaji huu utaifanya Tanzania kuwa tegemeo si tu kwa wananchi wake bali pia kwa mataifa yanayoizunguka" alisema Wolde.
.
Aidha, Wolde amesema kuwa Tanzania ni mshirika muhimu wa IAEA, huku shirika hilo likiahidi kuendelea kuunga mkono programu za saratani kupitia mafunzo kwa wataalamu na kusaidia upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dkt. Henry Humba, alisema serikali imeleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya kwa kuendeleza ujenzi wa kituo hicho, ambao umefikia asilimia 61.
.
"Mradi huo unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 30.4 na kukamilika Agosti 2026" alisema Dkt. Humba.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Prof. Najat Mohamed, amesema kuwa Tume hiyo itahakikisha kituo hicho kinakuwa salama kwa utoaji wa huduma za saratani huku ikiendeleza ushirikiano wa karibu na BMH.
Akimuwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma na Utafiti, Prof. Razack Lokina, amesema UDOM kwa kushirikiana na BMH watakitumia kituo hicho kuzalisha wataalamu wa kutosha wa saratani na kufanya tafiti zitakazosaidia kuboresha mikakati ya taifa ya kupambana na ugonjwa huo.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

