MIAKA 60 YA MUUNGANO,TUMEDHAMIRIA KUONDOA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WAOMBAJI WA FURSA ZA AJIRA NCHINI -WAZIRI SIMBACHAWENE
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Mhe.George Simbachawene amesema katika kipindi hiki cha miaka 60 ya muungano,Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imedhamiria kuondoa changamoto nyingi zinazowakabili waombaji wa fursa za ajira nchini kwa kuendesha usaili wa kuandika/mchujo Kidijitali kwa lengo la kuwafikia waombaji wote mahali popote walipo Tanzania bara na Zanzibar.
.
Simbachawene ameyasema hayo leo April 15,2024 alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuelekea katika Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.
.
Amesema kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kutambua kuwa Skauti ni suala la Muungano, TAKUKURU kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) ziumeunda timu ya uratibu ya kitaifa yenye Wajumbe kutoka Chama cha Skauti Tanzania (CST), ZAECA na TAKUKURU ili kuimarisha ushirikiano katika jitihada za kupambana na rushwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
.
Waziri Simbachawene amesema Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini,TASAF Awamu ya Tatu kwa sasa inatekeleza Kipindi cha Pili cha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambacho kinafanyika katika Mamlaka ya maeneo ya utekelezaji 186 ya Tanzania Bara na Zanzibar yakihusisha Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji ya Tanzania Bara na Unguja na Pemba kwa upande wa Zanzibar.
.
"Lengo ni kuziwezesha Kaya za Walengwa kutumia fursa za kuongeza kipato, kutumia huduma za Kijamii na Kiuchumi na kuwekeza katika kujenga na kuendeleza watoto wao ambao ni rasilimaliwatu" alisema Simbachawene.
Kwa upande mwingine, Simbachawene amesema katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano, mpango huo umekuwa na manufaa makubwa mathalani katika eneo la Uhawilishaji wa Ruzuku kwa Walengwa ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 824.4 kililipwa kwa Kaya Maskini 1,321,098 Tanzania Bara na Shilingi bilioni 41.2 ililipwa kwa Kaya Maskini 50,818 Zanzibar ili kuziwezesha kumudu gharama za msingi za maisha na kupeleka watoto wao shule na kliniki.
.
Aidha, Waziri Simbachawene amesema kumekuwa na mpango wa kuendeleza na kuboresha miundombinu ya huduma za jamii ambapo miradi 77 ya kuendeleza miundombinu katika sekta ya Elimu, Afya na Maji yenye thamani ya shilingi bilioni 3.6 imetekelezwa katika Halmashauri 50 za Tanzania Bara wakati miradi 20 yenye thamani ya shilingi bilioni 2.9 imetekelezwa Pemba na Unguja kwa lengo la kuimarisha miundombinu ya huduma za jamii katika maeneo husika
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

