WATANZANIA WAMETAKIWA KUULINDA NA KUUTUNZA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dkt.Suleiman Jafo amewataka Watanzania wote kuulinda na kuutunza Muungano kwa gharama kwani ni wa kipekee Afrika na Duniani.
Waziri Jafo ametoa rai hiyo leo Machi 26,2024 jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni kuelekea miaka 60 ya Maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
"Natoa rai kwa Wananchi wote wa Tanzania kuendelea kuuenzi, kukulinda na kuutunza Muungano wetu adhimu, ambao umedumu kwa miaka 60. Huu ni muungano wa kipekee barani Afrika na duniani kwa ujumla". alisema Jafo.
Sambamba na hayo, Waziri Jafo ametaja mafanikio yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali ikiwemo kiuchumi,kijamii na Mazingira ambapo huku kote kumekuwa na mafanikio makubwa sana.
"Ndugu Wanahabari;Tangu kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza na kuratibu shughuli ya hifadhi na usimamizi wa Mazingira ili kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali asili na maendeleo endelevu kwaajili ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho" alisema.
Dkt.Jafo amesema Idara ya Mazingira ilianzishwa mwaka 1992 ikiwa ni juhudi za Serikali kuhimiza uhifadhi na usimamizi wa Mazingira nchini kama ilivyohimizwa na Azimio la Rio mwaka 1992 linalozitaka nchi zote duniani kutambua uhusiano uliopo kati ya maendeleo na mazingira.
Aidha,Waziri Jafo amesema kufuatia kuanzishwa kwa Idara ya Mazingira, Tanzania iliridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayohusu Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira,ambapo katika kutekeleza Azimio la Rio la Mwaka 1992, Tanzania iliandaa Mpango wa Kwanza wa Taifa wa Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (National Environmental Action Plan –(NEAP) mwaka 1994.
Maadhimisho hayo ya Muungano hufanyika kila mwaka ifikapo tarehe 26 mwezi wa 4.
#JordanMediaupdates
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

