WAZIRI CHANA: UKATILI WA KIJINSIA HUSABABISHWA NA WATU WETU WA KARIBU
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Balozi Dkt.Pindi Chana(Mb) ametoa wito kwa taasisi na vyombo vya serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali nk. kuweka nguvu ili kuweza kukabiliana na janga la kimataifa la ukatili dhidi ya Wanawake na wasichana.
.
"Kwa wadau wa maendeleo,niwaelekeze muongeze ushirikiano ya muda mrefu na usaidizi kwa kuunga mkono jitihada za serikali katika kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia miongoni mwa jamii" amesema.
Dkt.Chana ameyasema hayo leo Disemba 6,2023 alipokuwa akifungua Kampeni ya Siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia tukio lililofanyika katika Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) Jijini Dodoma.
Amesema katika matukio mengi ya ukatili wa kijinsia wahanga wakubwa ni wanawake na watoto ingawa hata wapo wanaume, na takwimu za wanaume wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia zimekuwa zikiongezeka hivyo kama jamii tunapaswa kuchukua hatua madhubuti ili kukomesha janga hilo.
.
"Wanaodaiwa kufanya vitendo hivyo mara nyingi ni ndugu zetu wa karibu na ni wale tunaowaaamini sana katika familia na jamii zetu kwa ujumla. Ndani ya familia unakuta kuna mjomba,kaka,shangazi wanafanya Ukatili wa kijinsia" amesema Dkt.Chana.
Waziri Chana ameyataka mashirika yanayotetea haki za wanawake na watoto kujikita zaidi katika maeneo ya pembezoni kwani huko ndipo kwenye changamoto zaidi.
.
Amesema kama wadau wanapaswa kuwajibika katika kuimarisha ulinzi wa makundi maalum hususani wanawake na watoto, sisi sote tunaweza kupinga mazoea mabaya ya kiutamaduni na kijamii ambayo yanadhoofisha haki za wanawake na watoto.
.
Aidha, Dkt.Chana amesema takwimu zinaonesha uwepo wa ongezeko la matukio ya ukatili huo hapa nchini, na ongezeko hilo linatokana na sababu mbalimbali ikiwemo jamii kuwa na uelewa juu ya madhara yatokanayo na ukatili wa kijinsia na kutoa taarifa za ukatili huo katika madawati ya kijinsia.
.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha UDOM Prof.Lughano Kusiluka amesema chuo hicho kimefanikiwa kuanzisha dawati la jinsia (Gender Desk)ambapo lilizinduliwa mwaka 2022 na lengo kuu la dawati hilo kutokomeza ukatili wa kijinsia katika jamii ya chuo kikuu cha UDOM.
.
"Dawati hili linahudumia wana jamii wote pamoja na wafanyakazi na wanafunzi, walimu na taasisi zilizopo katika Chuo Kikuu Cha Dodoma na wanaotuzunguka. kupitia dawati hili, Chuo Kikuu Cha UDOM kimefanikiwa kutoa elimu na kupinga masuala ya ukatili wa kijinsia ndani na nje ya jamii yetu" amesema Kusiluka.
.
Aidha, Prof.Kusiluka amesema changamoto mbalimbali zinazokwamisha kuondokana na suala la ukatili wa kijinsia katika jamii yetu ni uelewa mdogo wa wadau juu ya ukatili wa kijinsia,kutotoa taarifa kwa wakati kipindi ukatili wa kijinsia unapojitokeza na kuendelea kuwepo kwa mila potofu zinazoamasisha ukatili wa kijinsia katika jamii yetu ya Tanzania.
#JordanMediaupdates
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

